TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA KUHAMISHA MAKABURI

September
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC hivi karibuni limeendelea na zoezi la ulipaji fidia kama kifuta machozi kwa ndugu wa marehemu sita katika mtaa wa Kifuru kata ya Kinyerezi Manispaa ya Ilala Jijini Dar Es Salaam kufuatia zoezi la kuhamish makaburi kupisha mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme wa reli ya kisasa - SGR Septemba 08, 2021.
Makaburi hayo sita yamehamishwa kutoka mtaa wa Kifuru uliopo kata ya Kinyerezi manispaa ya Ilala na kwenda katika Makaburi ya Halmashauri yaliyopo kata ya Segerea - Ilala Dar es Salaam kwa lengo la kupisha uwekaji wa nguzo za umeme katika ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Zoezi hilo limeshirikisha Maafisa kutoka shirika la Reli Tanzania, Maafisa Afya wa Manispaa ya Ilala, Mtendaji wa Kata hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Maafisa wa Polisi, ndugu wa marehemu na viongozi wa dini ili kuhakikisha ndugu wa marehemu wanapata stahiki yao na na kuhakikisha mradi unaondelea wa ujenzi wa Reli ya Kisasa haupati kikwazo katika ujenzi.
Akiongea katika zoezi hilo afisa mwandamizi kutoka Shirika la Reli Tanzania Bwana Ramadhani Mfwikira amesema zoezi hilo ni endelevu ili kuhakikisha wananchi wanaostahili wanapata malipo kwa makaburi hayo sita.
Aidha, mmoja wa ndugu wa marehemu Bibi Salma Saidi Mohammed alisema ameridhia zoezi hilo lifanyike kwakua maendeleo ya nchi ni ya wote hivyo basi ni jukumu la kila mmoja kushirikiana na serikali katika kutimiza lengo la maendeleo.