Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA FIDIA MKOANI TABORA


news title here
30
August
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha nne Tabora - Isaka hivi karibuni Agosti, 2023.

Wananchi takribani arobaini na moja katika kijiji cha usongwahala kilichopo wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamekabidhiwa malipo yao na kupewa notisi ya siku kumi na nne ili waweze kumpisha mkandarasi kuendelea na ujenzi wa SGR.

Mthamini kutoka TRC Bw. Valentine Baraza alisema kuwa maeneo yaliyotwaliwa ni kwaajili ya ujenzi wa njia kuu ya reli ya SGR ambapo wananchi wote waliopitiwa na mradi walifanyiwa uthamini na kutoa taarifa zao kwa kushirikiana na mtendaji pamoja na mwenyekiti wa kijiji.

“Tunashirikiana na uongozi wa kijiji husika ili kuhakikisha taarifa za mfidiwa sababu wao ndio wanaojua wananchi wa eneo lao kiusahihi zaidi” alisema Bw. Baraza.

Pia Mwenyekiti wa kijiji cha Usongwahala Bw. Kayagira Kajuba ametoa shukrani kwa serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwathamini wananchi kwa kuwapatia fidia kwa wakati na kusema kuwa kupitia malipo hayo mwanakijiji ataweza kujiendeleza katika kilimo na biashara mbalimbali.

“Watu watajenga nyumba za kisasa na biashara zitaongezeka kwa kasi zaidi” alisema Bw. Kajuba.

Mwananchi kutoka kijiji cha Usongwahala Bw. Kasepa Maganga alisema kuwa kupitia malipo ya fidia atajikwamua kiuchumi na kubadilisha maisha kwa kujenga nyumba ya kisasa na kuongeza mashamba.

Zoezi hilo la ulipaji fidia ni endelevu ambapo serikali kupitia TRC inahakikisha wananchi wote waliotwaliwa maeneo yao wanapatiwa stahiki zao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kiujumla.