TRC YAENDELEA NA UTOAJI ELIMU KATIKA WIKI YA USALAMA WA RELI
October
2022
Shirika la Reli Tanzania linaendelea na kampeni ya uelewa kuhusu ulinzi na usalama wa reli katika maeneo ya ushoroba wa reli jijini Dar es Salaam Oktoba 11, 2022.
Zoezi hilo la uhamasishaji ni katika kuadhimisha wiki ya usalama wa reli kupitia vyama vya reli Kusini mwa Afrika - SARA (South African Railway Association) ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 10 - 13.
Aidha, kampeni hiyo iliyobeba kauli mbiu "CHUKUA TAHADHARI,TRENI ZINAMWENDO WA HARAKA ,NI HATARI" imelenga katika kuelimisha jamii nzima kuelewa na kuheshimu Sheria na kanuni za ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli.
Afisa wa Jamii kutoka Shirika la Reli Tanzania Bwana Leodgard Otaru amesema kuwa usafiri wa reli ni usafiri wenye usalama wa kiwango cha juu zaidi duniani ukilinganisha na njia nyingine za usafirishaji hivyo ni muhimu kwa jamii kuheshimu Sheria na kanuni zilizowekwa ili kuzuia madhara yatokanayo na kutozingatia Sheria.
"Ndugu wananchi wenzangu niwahakikishie kuwa usafiri wa reli ni usafiri wenye kuzingatia usalama zaidi ukilinganisha na aina nyingine ya usafiri duniani hivyo niwaombe tuwe watu wa kuheshimu Sheria za usalama zilizowekwa ikiwemo kuzingatia alama za reli na umakini kwenye vivuko kuepusha ajali zisizo za lazima " alisema Bwana Leodgard Otaru .
Bwana Otaru ameongeza kuwa viongozi wa serikali za mitaa wanapaswa kuwa mabalozi wazuri katika kusaidia Serikali kuwabaini wahujumu miundombinu ya reli kwa makusudi na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya reli na kuhatarisha usalama wa abiria na mali.
"Tunashukuru watu wa TRC kwa kutuletea elimu hii, elimu ni maendeleo kwasababu bila elimu jamii itaathirika, mimi kama mwenyekiti wa mtaa nitaendelea kuhamasisha wananchi waendelee kujitokeza katika mikutano ya hadhara kama hii ili kujenga utamaduni na kuwa na uelewa wa mambo mbalimbali yanayoleta maendeleo katika nchi" alisema Bwana Andrew Olutu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Karakata.
Naye Bwana Ernest Pius Mkaza kutoka Mtaa wa Karakata amewasihi wananchi wenzake kufuata kile ambacho wanaelimishwa kuhusu masuala ya usalama wa reli ili kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu ya kujenga nchi.
Ulinzi na usalama wa reli ni jukumu la kila mwananchi kutekeleza na kutoa ushirikiano kwa Serikali pale ambapo uvunjifu wa Sheria zilizowekwa unapotokea ili kuleta maendeleo.