Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTWAA ARDHI WILAYA YA KWIMBA - MWANZA


news title here
16
May
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la kuhamisha makaburi kwa awamu ya tatu kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza linalofanyika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza hivi karibuni Mei, 2022.

Takribani makaburi 210 yanahamishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kijiji cha Mwamuhembo, Malya, Kitunga, Isabilo pamoja na kijiji cha Goloma vilivyopo wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza.

Mthamini kutoka TRC Bw. Aristides Rwebangira alisema kuwa wananchi wanaendelea na kutoa ushirikiano wa kutoa maeneo ikiwemo sehemu walipohifadhiwa wapendwa wao.

Bw. Rwebangira alisema kuwa Shirika linafanya zoezi hilo la uhamishaji kwa kufuata taratibu zote za kisheria kwa kufanya uthamini wa kaburi pamoja na kushirikiana na viongozi mbalimbali akiwemo Afisa Afya wa wilaya, Afisa Ardhi wa wilaya, katibu tarafa, viongozi wa kijiji pamoja na viongozi wa dini.

“Tunahakikisha vibarua wote wanakua na vifaa katika ufukuaji” alisema Bw. Rwebangira.

Aidha, Bw. Rwebangira alisema kuwa makaburi hayo yanayohamishwa ni ya njia kuu itakopojengwa reli ya SGR pamoja na sehemu za kuchukua udongo.

Afisa Afya wa Wilaya ya Kwimba Bw. Gaspa Luziga ameeleza kuwa zoezi linaendeshwa kufuata taratibu zote za kiafya ili kuepusha maambukizi ama mripuko wowote wa magonjwa kwa wananchi.

“Wachimbaji wanapewa vifaa vya kujikinga pia tunamwagia dawa katika miili pamoja na sehemu ambayo mwili umetolewa” alisema Bw. Luziga.

Naye mtendaji wa kijiji cha Kitunga Bi. Happiness Canisio ameipongeza Serikali pamoja na Shirika la Reli Tanzania kwa kuendelea kusimamia vyema maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya vijiji kwa kuwapatia fursa katika mradi wa SGR.

“Wananchi ni waelewa na wanafurahi kufikiwa na maendeleo hasa miundombinu ya reli itakayorahisisha usafiri na vijiji kuzidi kukua” alisema Bi. Happiness.

Shirika la Reli linaendelea na zoezi la kuhamisha makaburi katika maeneo mbalimbali ambayo yamepitiwa na mradi wa reli ya kisasa kipande cha tano Isaka - Mwanza.

Tanzania Census 2022