Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTWAA ARDHI NZEGA - TABORA


news title here
03
October
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha nne Tabora - Isaka kwenye vijiji takribani tisa vilivyopo wilayani Nzega mkoa wa Tabora hivi karibuni Oktoba, 2023.

Mthamini kutoka TRC Bw. Valentine Baraza alisema kuwa zoezi hilo la utwaaji ardhi linaloambatana na uhamishaji wa makaburi limefanyika takribani kwenye vijiji tisa vikiwemo vijiji vya Luhumbo, Mahene, Ilole, Mwino, Kayombo, Malolo, Nawa, Usongwahala na Bukene.

“Makaburi hayo tuliyahamisha yalianishwa katika njia ya reli, pamoja na maeneo kwaajili ya kuchimba vifusi” alisema Bw. Baraza.

Aidha Bw. Baraza alieleza kuwa wananchi wametoa ushirikiano mzuri kwa kuonyesha sehemu ambazo makaburi yalipo wakishirikiana na viongozi wa kijiji, viongozi wa kata, viongozi wa dini pamoja na madiwani.

Naye Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Bernard Pilly alisema kuwa serikali ina fuata taratibu zilizowekwa katika utwaaji ardhi ikiwemo ufukuaji makaburi kwa kuhakiki idadi ya mabaki yaliyopatikana.

“Mimi kama Mthamini ni lazima nihakiki mabaki yaliyopatikana kwenye kila kaburi ili kuwaorodhesha wasimamizi wa makaburi hayo katika jeduali la fidia kwaajili ya kuwapitia kifuta machozi” alisema Bw. Pilly.

Hata hivyo Bw. Pilly alifafanua kuwa kifuta machozi katika kila kaburi ni sawa isipokuwa uthamini unafanywa katika kila kaburi ambalo litakuwa limejengewa na kufidia vitu vilivyowekwa katika kaburi la aina hiyo.

“Huwezi kufidia thamani ya binadamu hivyo ndio maana wananchi wanapatiwa kifuta machozi baada ya kufukua kutoka na wengine kuwa na udanganyifu wa kuonyesha sehemu pasipo na kaburi” alisema Bw. Pilly.

Mwenyekiti wa kijiji cha Usongwahala Bw. Kayagila Kajola alisema kuwa wanakijiji wametoa ushirikiano kwa kukubali wapendwa wao kuhamishiwa eneo jengine ili kupisha ujenzi huo wa SGR kwa manufaa ya wanakijiji na taifa.

Mradi wa ujenzi wa SGR unaendelea katika maeneo mbalimbali ambapo kwa kipande cha nne Tabora - Isaka umefikia asilimia 4.65.