Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTWAA ARDHI KWA WANANCHI KUPISHA NJIA YA UMEME MRADI WA SGR


news title here
28
October
2022

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la kuhamasisha wananchi kuhusu utwaaji ardhi ili kupisha ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora linalofanyika katika Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro hivi karibuni Oktoba, 2022.

Zoezi hilo la utwaaji ardhi linahusisha Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma Jiji na Chamwino mkoani Dodoma na Wilaya ya Mvomero na Kilosa Mkoa wa Morogoro ambapo takribani makaburi 179 yanatarajiwa kuhamishwa ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme.

Afisa maswala ya Jamii kutoka TRC Bw. Leodgard Otaru amesema kuwa takribani makaburi 179 katika mitaa na vijiji 20 yatahamishwa na kwenda kuzikwa sehemu maalumu iliyoandaliwa na Serikali za mitaa na vijiji ili kupisha ujenzi huo.

"Zoezi hili linaendelea vizuri na zaidi ya makaburi 179 yanatarajiwa kuhamishwa katika awamu hii na kwenda kuzikwa sehemu maalumu iliyotengwa na Serikali ya mitaa na vijiji husika ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme ya SGR" alisema Bw. Leodgard Otaru .

Bw. Leodgard Otaru ametaja Mitaa na vijiji vitakavyohusika kwenye zoezi hilo la uhamishaji ni Kimagai, Msagali, Chololo, Kikombo, Iyumbu, Miganga, Ntyuka, Zuzu, Kimambila, Chimwaga, Igandu, Mnase, Behewa, Chanzuru, Kibaoni, Kichangani, Kondoa, Mbumi, Munisagara na Mwasa hivyo kuwataka wananchi watoe ushirikiano ili kutimiza lengo lilokusudiwa.

Naye Afisa Mtendaji Kijiji cha Kibaoni Bw. Dicksoni Eliakimu ameeleza kuwa zoezi hilo limeweza kuwafanya wananchi kutambua umuhimu wa kuzika kwenye maeneo maalumu yaliotengwa na Serikali ambapo inatoa fursa kwa matumizi bora ya ardhi na kuepusha usumbufu pindi miradi mikubwa ya kimaendeleo inapotekelezwa .

"Zoezi hili ni zuri sana kwani linawafahamisha wananchi sehemu hiyo haitakiwi kuzikwa tena imetengwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali, wananchi sasa wanatakiwa wazike sehemu maalumu zilizotengwa" amesema Bw. Dicksoni Eliakimu.

Kwa upande mwingine zoezi hili la utwaaji ardhi limetoa fursa za ajira kwa vijana wengi ambapo kwa siku takribani vijana 50 wanashiriki katika zoezi la kuhamisha makaburi na kulipwa stahiki zao kama vibarua.

Zoezi hilo la kuhamisha makaburi linafanyika kwa umakini na hatua zote za kiafya zinafuatwa kwa kuwashirikisha maafisa afya, viongozi wa dini, viongozi wa serikali ya mtaa pamoja na wananchi wa eneo husika.