Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTWAA ARDHI KUPISHA UJENZI WA SGR NYAMAGANA MAGHARIBI - MWANZA


news title here
06
January
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza linalofanyika katika mtaa wa Nyamagana Magharibi jijini Mwanza hivi karibuni Januari, 2023.

Zoezi hilo la utwaaji ardhi linaambatana na uhamishaji wa makaburi ya Umoja wa Hindu wa mkoa wa Mwanza wakiwemo dhehebu la Baniani na Shia yaliyopo katika eneo hilo la Nyamagana Magharibi.

Msimamizi wa SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza Mhandisi Blasius Mwita alisema kuwa zoezi la utwaaji ardhi linafuata Sheria za serikali za ujenzi wa reli kwa kuchukua eneo ambalo njia ya reli inapita pamoja na kufuata taratibu zote za makabidhiano ya ardhi.

“Popote ambapo reli itapita mkandarasi akihitaji eneo, tunafuata taratibu kulipata ili tumkabidhi mkandarasi aendelee na ujenzi” alisema Mhandisi Mwita.

Naye Msimamizi wa Taasisi ya Hindu (Hindu Union Crematorium) Bw. Mohan Mishu ameeleza taasisi imeridhia kufanya zoezi hilo ili kupisha maendeleo ya Serikali na wananchi.

“Taasisi hii ndio inayosimamia makaburi yote, imani yetu wahindi tukishazika taasisi ndio inayoachiwa mamlaka yote ya kusimamia wapendwa wetu “ alisema Bw. Mohan.

Hata hivyo kwa upande wa dhehebu la Shia taasisi imeomba kutoa muda wa ziada kwa kuwaruhusu ndugu kuja kufanya dua na mila mbalimbali kutokana na utofauti wa kiimani wa dhehebu la Shia kwenye maziko kwa kuzika miili kamili na dhehebu Baniani kufanya maziko kwa kuchoma na kuzika mabaki ya majivu.

Zoezi hilo linaendelea kufanyika kwa kusimamiwa na timu kutoka TRC, wataalamu wa afya pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi wa dini wa madhehebu husika.