Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU USALAMA WA RELI KWA WANANCHI


news title here
30
November
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la uhamasishaji na utoaji elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya reli zikiwemo shule na taasisi mbalimbali kutoka Dar es Salaam hadi Soga katika kipande cha kwanza cha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR, Novemba 2023.

Zoezi la utoaji elimu limeanzia katika kata ya Buguruni kwa Madenge, shule ya msingi Majani ya chai, shule ya sekondari Ilala, shule ya sekondari majani ya chai, wananchi wa mtaa wa stakishari ,wakazi wa uwanja wa ndege katika kata ya kipawa, Kamata Stesheni pamoja na buguruni kwa Madenge wilaya ya Ilala.

Afisa Usalama wa reli kutoka Kitengo cha Usalama wa reli Mhandisi Chisondi Maingu amesema lengo la zoezi ni kuwaelimisha wananchi na wanafunzi umuhimu wa kufuata sheria na taratibu wanazoelimishwa namna ya kuzingatia Sheria za Usalama wa reli ikiwemo kutokugusa nyaya za umeme zilizopo reli ya kiwango cha kimataifa ( SGR), wasitembee kwenye uzio wa reli ya Umeme, watumie vivuko vilivyowekwa kwaajili ya kuvuka kwenye makutano na reli ya SGR na barabara, kufuata sheria za uvukaji wa Barabara katika makutano ya barabara na reli, kutokupanda treni na kushuka wakati treni ikiwa kwenye mwendo.

"Tukumbuke kua umeme unaotumika kuendesha treni ya SGR ni umeme mkubwa wa Volt 25000 huu ni umeme mkubwa sana kwahiyo tunaomba mzingatie sheria zote za Usalama tunazowapatia" ameongeza Chisondi.

Kamishina wa Polisi - Polisi Jamii Reli Fadhili Eshakazoba amewataka wananchi na wanafunzi kulinda miundombinu ya reli ya kisasa na kuchukua tahadhari ili iweze kutumia katika usafirishaji wa abiria na mizigo kwani utakua usafiri wa haraka na salama.

"Kama Babu zetu wameweza kulinda miundombinu ya reli ya zamani ( reli ya kati ) kwanini sisi tusiilinde miundombinu hii ya kisasa Ili tuweze kunufaika na vizazi vijavyo nao waikute waitumie kwahiyo hapa Kila Mmoja awe balozi wa kuilinda reli hii na kuchukua tahadhari pindi avukapo makutano ya barabara na reli." amefafanua ACP. Fadhili.

Balozi wa Shina la Buguruni kwa Madenge Bw. Mshindo Abasi amewashukuru TRC kwa kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi na kufanya shughuli karibu na maeneo ya reli kwani itasaidia kuchukua tahadhari na kuzingatia Usalama.

"Umeme huu ni mwingi na unajumuisha vitu vingi zikiwemo nyaya kupitia elimu hii hata tukiona nyaya imekatika hakuna mwananchi atakayeshika bali tutapiga simu TRC kwaajili ya huduma ya haraka" ameongeza Mshindo Abasi.

Shirika la Reli Tanzania limekua na zoezi endelevu la utoaji elimu ya Usalama katika maeneo yote ilikopita reli ya kiwango cha kimataifa - SGR na reli ya kati - MGR kwa wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao karibu na reli na katika stesheni zote zinazosimamiwa na TRC.