Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAADHIMISHA KILELE CHA WIKI YA USALAMA WA RELI


news title here
13
October
2022

Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia – TAZARA, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini – LATRA, Wakala wa Barabara Tanzania – TANROADS, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini – TARURA wameadhimisha kilele cha wiki ya usalama wa reli Kamata jijini Dar es Salaam Oktoba 13, 2022.

Aidha, Wiki ya Usalama wa reli huadhimisha tarehe 10 hadi 13 mwezi Oktoba kila mwaka kwa wanachama wa vyama vya reli kusini mwa Afrika (SARA) ikiwa na lengo la kuendelea kusisitiza na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa reli. Mwaka 2022 Tanzania imekuwa mwenyeji ambapo kaulimbiu ni “CHUKUA TAHADHARI, TRENI ZINA MWENDO WA HARAKA, NI HATARI”.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mgeni rasmi Mhe. Atupele F. Mwakibete Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua vyema umuhimu wa ulinzi na usalama wa miuondombinu ya reli ndiyo maana inaendelea kutoa fedha kujenga na kuboresha miundombinu ya reli ili kuwezesha uendeshaji wa shughuli za reli.

Sambamba na hivyo, Mhe Waziri ametoa wito kwa wafanyakazi wa TRC na Taasisi zingine wajiendeleze kwa kutoa mafunzo ili kuwapa ujuzi waumishi, “nilivyokua napita kwenye mabanda nimeona TRC na LATRA wamepeleka vijana wao nje kupata elimu na ujuzi mpya kwahiyo na taasisi zingine ziige taasisi hizi ili kuweza kuendesha na kusimamia miradi mikubwa kama SGR’’ amesema Mhe. Atupele.

Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini CPA Habibu Suluo amesema LATRA na TRC ni washirika wa SADC, katika siku hii ya kilele cha wiki ya usalama wa reli ametoa wito kwa watumiaji wa reli wakiwemo wananchi na wadau kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika kulinda miundombinu ya reli vilevile watumishi kufanya kazi kwa weredi katika kuzingatia Sheria za kazi za reli ikiwemo kuhakikisha usalama wa behewa, vichwa vya treni kabla havijaanza safari na vikiwa safarini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TAZARA Eng. Bruno Ching’andu amesema kuwa kila mtu afikirie kuhusu usalama wake na wenzake kwa kutumia elimu inayotolewa kwani inasikitisha kuona kwamba kila mwaka zaidi ya watu 35 barani Afrika wanapoteza maisha kutokana na ajali ndogo za treni inayotokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu usalama wa reli.

“Watu hawajali kabisa kuhusu ulinzi na usalama wao, hawajishughulishi wala kuchukua tahadhari, wanaamini treni inawaona na itasimama, hii ina sikitisha sana, kila mwaka zaidi ya watu 35 Afrika wanapoteza maisha kutokana na ajali ndogo za treni, hii ni hatari inabidi jamii ieleweshwe na kupewa elimu ya masuala ya usalama” amesema Eng. Bruno Ching’andu.

Mkurugenzi Mkuu TRC, Masanja Kadogosa aliwashukuru wananchi, wafanyakazi wa TRC na umma kwa ujumla kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika jitihada zinazofanywa kuhakikisha miundombinu ya reli inakuwa salama.

Mkurugenzi Mkuu TRC, aliongeza kuwa “Katika kuadhimisha wiki hii wananchi wameonesha ushirikiano mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano iliyoandaliwa kwaajili ya kutoa elimu ya uelewa kuhusu usalama wa reli. Niwasihi waendelee kuwa mabalozi kwa kuwapatia elimu hiyo wananchi wengine”.