TRC TAYARI KUSAFIRISHA MIZIGO KUTOKA BANDARINI MPAKA BAHI
May
2026
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara, Mei 18, 2026, ametembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa kipande cha Reli kinachounganisha na Bandari ( Portlink), Stesheni za mizigo Morogoro na Stesheni ya Bahi, Dodoma.
Ziara ya Katibu Mkuu Uchukuzi imelenga kukagua na kujionea utayari wa TRC kuanza usafirishaji mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda, Morogoro, Ihumwa na Bahi, kisha maeneo mengine ya nchi na nje ya nchi.
Akiwa Port Link, Profesa Kahyarara, amesema, "yani reli ya SGR inaingia mpaka eneo la Malindi, ambapo mizigo itapakiwa na kusafirishwa kwa treni ya mizigo ya SGR mpaka Bahi ambapo mizigo hiyo itafaulishwa na kupakizwa kwenye reli ya MGR kisha kusafirishwa kuelekea maeneo mengine ya nchi na nje ya nchi. Aidha, serikali kupitia TRC imewekeza katika ujenzi huo wa kimkakati kwa lengo la kuiwezesha bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa ufanisi kwa kupunguza mrundikano wa mizigo, kupunguza foleni ya magari katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na mwisho kuondoa foleni ya malori yanayotoka bandarini kuelekea barabara ya Morogoro.
Kitendo cha reli ya SGR kuchukua mizigo bandarini na kuisafirisha mpaka Bahi italeta mafanikio makubwa sana ikiwemo kuongeza mapato ya nchi na kwa mafanikio haya Tanzania itakuwa kinara wa usafirishaji Afrika Mashariki" Amesema Mhe.Prof.Kahyarara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Mha. Machibya Shiwa, amesema, kukamilika kwa eneo la portlink lenye ukubwa wa mita za mraba laki moja ( 100000) utaruhusu upakiaji mizigo kwa haraka kutoka bandarini, mizigo kutoka kwenye malori na mizigo kutoka bandari kavu za watu na kampuni binafsi ( private ICDs) hii itaongeza ufanisi wa bandari katika kuhudumia wateja.
Katika hatua nyingine, Elitunu Mallamia Mkuu wa Uhusiano na Uratibu kutoka kampuni ya uwekezaji bandari ya Dar es Salaam ya DP World, amesema kampuni hiyo iko tayari kushirikiana na kuwekeza katika kuhakikisha miundombinu ya reli inakidhi hadha ya ongezeko la mizigo ili mizigo isafiri kwa haraka.
Bwana Elitunu ameongeza kuwa ni wakati wa wadau wa sekta ya reli wakiwemo wamiliki wa malori, wasafirishaji na wafanya biashara washiriki kikamilifu kuhakikisha sekta ya reli inakua ili kuboresha huduma za usafiri.
Mafanikio ya ujenzi wa miundombinu ya reli itaifanya Tanzania kuwa kinara wa usafirishaji mizigo Afrika Mashariki.

