Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC NA WFP KUSHIRIKIANA KUSAFIRISHA BIDHAA ZA MAZAO YA MATUNDA NA MBOGAMBOGA


news title here
11
October
2022

Shirika Reli Tanzania – TRC na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP wamezindua mpango wa makubaliano ya kutoa huduma ya usafirishaji wa bidhaa za mbogamboga na matunda, makao makuu WFP Jijini Dar es Salaam, Oktoba 10, 2022.

Aidha, katika kuendelea na mashirikiano, mashirika haya mawili yameingia katika makubaliano ya kutoa huduma ya usafiri wa bidhaa za mbogamboga na matunda katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam kwa kuanzia.

Mkurugenzi Mkuu TRC, Masanja Kadogosa amesema kuwa Machi, 2022 TRC na WFP walifanya utafiti kwa lengo la kupata ufumbuzi na mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kuzuia hasara baada ya kuvuna. Madhumuni mengine ya utafiti huo ni pamoja na kutafuta usafiri upi ni wa uhakika, salama na wa gharama nafuu.

Hata vivyo Mkurugenzi Mkuu TRC alisema kuwa kuna matarajio makubwa katika mradi utakapoanza kutekelezwa kwanza utapunguza uharibifu wa mazao baada ya kuvunwa na kuimarisha uzalishaji ikiwemo na usambazaji katika masoko ya ndani na nje ya nchi kwa kutumia usafiri wa reli.

“Leo tunachukua hatua nyingine muhimu ya ushirikiano kati ya Shirika la Reli Tanzania na Shirika la Mpango wa Chakula duniani. Mahusiano yetu katika usafirishaji wa chakula cha msaada kwenda maeneo mbalimbali yamedumu kwa zaidi ya miaka 24. Ushirikiano huu umesaidia katika kuboresha utendaji kazi wa mashirika yote hususani katika kuhakikisha jamii inanufaikia kupitia mashirika haya” alisema Mkurugenzi Mkuu TRC.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu WFP Tanzania Bi. Sarah Gibson amebainisha kuwa usafirishaji wa bidhaa za matunda na mbogamboga zitawasaidia wakulima kuinuka kiuchumi pamoja na upatikanaji wa ajira kwa wingi.

“Ninafuraha siku ya leo kwa kuzindua mradi wa Pamoja kati ya Shirika la reli Tanzania na Shirika la Mpango wa chakula duniani katika usafirishaji wa mbogamboga na matunda, mradi huu utafaidisha wakulima na kutuhakikishia upatikanaji wa chakula bora, mradi huu pia utatoa ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini katika jamii” alisema Mkurugenzi Mkuu WFP Tanzania.