Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC NA WFP IMEPOKEA TAARIFA YA UTAFITI WA USAFIRISHAJI WA MAZAO YA MBOGAMBOGA NA MATUNDA


news title here
03
March
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP limepokea taarifa ya utafiti wa usafirishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda kwa njia ya reli kutoka katika Kampuni ya Innovex Development Consultant Limited kwenye kikao kifupi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya TRC jijini Dar es Salaam Machi 2, 2023.

Utafiti umefanywa kwa ushirikiano kati ya TRC na WFP kwa lengo la kukuza uchumi kupitia kilimo cha mazao madogo ikiwemo zao la Nyanya, Vitunguu na Kabichi.

Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa ameeleza kuwa TRC wamejipanga vyema kusafirisha aina ya mazao hayo kwa kuyahifadhi katika mabehewa ambayo yataandaliwa kwaajili ya kusafirisha mazao katika mikoa mbalimbali.

“Mabehewa yatakuwa na majokofu kwaajili ya kutunza ubaridi ili zao kama nyanya ama embe yasiharibike kabla ya kufika katika eneo husika” alisema Ndugu Kadogosa.

Aidha, Ndugu Kadogosa alisema kuwa TRC ni taasisi ambayo inafanya biashara na imejikita katika kutoa huduma kwa wananchi wote hasa kwa watu wenye hali za kawaida hivyo kupitia mpango huo utawanufaisha wakulima wadogo hasa vijana ili kuingia katika kuwekeza katika maeneo ambayo yamelengwa kwa kufanyia kazi katika hatua ya kwanza ya mpango huo.

“Maeneo ambayo tutaanza nayo ni kati ya Kilosa, Gulwe, Mpwapwa hadi kuja na Dar es Salaam” alisema Ndugu Kadogosa.

Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Bi. Sarah Gibson alisema kuwa mpango huo wa usafirishaji wa mbogamboga na matunda ambao umejadiliwa kwa kipindi kirefu unalenga kukuza kipato pamoja na uzalishaji hasa wa mazao madogo.

“Huu mpango utajumuisha sekta binafsi, taasisi pamoja na watu binafsi kujiunga na kilimo na vilevile kusafirisha kwa usalama na bei nafuu” alisema Bi. Sarah.

TRC na WFP ni wadau wanaoshirikiana katika mambo mbalimbali ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza pato la taifa kupitia usafirishaji wa bidhaa kwa njia ya reli.