Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC NA TPSF WAFANYA KONGAMANO LA KWANZA LA WADAU KUJADILI FURSA KATIKA MRADI WA SGR


news title here
30
January
2021

Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kushrikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini – TPSF wamefanya kongamano la kwanza la wadau wa sekta binafsi kujadili fursa katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Mwanza – Isaka katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza Januari 30, 2021.
Lengo la Kongamano hilo ni kuandaa mpangokazi wa ushirikishwaji wa Sekta binafsi nchini katika mradi huo unaotarajiwa kuanza utekelezaji wake hivi karibuni ambapo Mkandarasi kutoka China kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation pamoja na China Railway Construction Company watatekeleza mradi huo.
“Leo tumekutana hapa kujadili ujenzi wa reli ya kisasa na jinsi tutakavyonufaika nao” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Bwana Francis Nanai
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela ambapo wadau kadhaa wa sekta binafsi wakiwemo wasafirishaji, watoa huduma za fedha, wakulima, wafugaji, wavuvi, kampuni za uzalishaji, viwanda, wakandarasi na wajasiriamali wadogo wadogo walihudhuria kongamano hilo.
Wadau wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Bodi ya Usajili Wahandisi Nchini, Ofisi ya Usharoba wa Kati, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Bodi ya Usajili Wakandarasi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa Kongamano hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha sekta binafsi zinashirikishwa katika miradi mikubwa ya kimkakati ili kukidhi makubaliano ya kimkataba katika miradi na kuleta manufaa kwa taifa
Kadogosa aliongeza kuwa “Ujenzi huu wa kipande cha tano ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi, mradi huu ni mkubwa sana na nina uhakika karibu Trilioni moja itabaki hapa nchini kupitia fursa zitakazopatikana”
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPSF Bi. Angelina Ngalula ameishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutengeneza fursa kupitia miradi ya kimkakati ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutuletea fursa, sisi wadau ni vyema tukajipanga kushiriki wakati wa ujenzi na kuutumia mradi huu utakapokamilika” alisema Bi. Angelina Ngalula
Bi. Ngalula aliongeza kuwa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi ni muhimu kwani hata Mhe. Rais anatambua ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maenedeleo na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hivyo wadau wa sekta binafsi wanatakiwa kuyabeba maono ya Mhe. Rais na kuyafanyia kazi.
Wadau walipata fursa kuuliza maswali na kupata majibu, pia waliweza kutoa maoni juu ya namna ya upatikanaji wa taarifa za fursa za kibiashara katika mradi huo. Kongamano hili linakuwa la kwanza kufanyika nchini kwa lengo la kujadili namna sekta binafsi zitakavyoshiriki katika miradi ya kimkakati nchini.