Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC NA JKCI KUTOA HUDUMA YA VIPIMO VYA MOYO BURE KWA ABIRIA WA SGR


news title here
18
September
2026

Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), zinatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya Moyo na yasiyoambukiza kwa abiria wa SGR, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani Septemba 29.

Huduma hiyo inatarajiwa kufanyika Septemba 21 hadi 27, 2026 ambapo wananchi watakaotumia usafiri wa SGR watapata fursa ya kupimwa afya ya moyo bila malipo katika kipindi hicho.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge, amesema hatua hiyo inalenga kufikia wananchi kwa urahisi zaidi na kuhakikisha wanapata huduma za afya, upendo na matumaini ya kuishi.

Dkt. Kisenge amesema gharama za vipimo vya magonjwa yasioambukiza inaweza kufika kiasi cha Tsh. 500,000 hospitali lakini kupitia TRC na JKCI abiria watakaofika stesheni kukata tiketi na watakaosafiri na treni watapata huduma ya vipimo bure na kwamba hii haijawahi kutokea Duniani kuwa na treni inayotoa huduma kama hizi katika safari.

“Tunataka kuhakikisha wananchi wanapata upendo na matumaini ya kuishi. Tutakuwa na huduma za upimaji wa moyo na magonjwa yasiyoambukiza ndani ya SGR, na mtu atakayebainika kuwa na tatizo atachukuliwa hatua za matibabu,” amesema.

Aidha, mpango wa kuwa na huduma za hospitali ndani ya treni hauishii katika maadhimisho hayo, bali unalenga kuwa huduma endelevu kwa wananchi wanaosafiri kwa SGR.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema wanaendelea kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya ndani ya treni, ikiwemo kufanya marekebisho maalumu katika baadhi ya mabehewa.

Amesema mpango huo unaweza kusaidia wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine, kwa kuwa mabehewa hayo yatakuwa na vitanda na mazingira ya kuwezesha wagonjwa kuendelea kupata huduma wakati wa safari.

“Tunajaribu kuangalia mazingira ya hospitali zetu na namna mabehewa yanavyoweza kufanyiwa marekebisho ili kusaidia wagonjwa wanaosafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, Mabehewa yanaweza kuwa na vitanda na wagonjwa wakaendelea kupata matibabu tofauti na kusafirishwa kwa magari ya wagonjwa,” alisema. Mha. Machibya.

Alisistiza kuwa mpango huo unalenga pia kuunganisha usafiri wa reli na huduma za afya, huku wananchi wakipewa fursa ya kupata uchunguzi wa afya bila kulazimika kusubiri hadi wafike hospitalini.