TRC MSTARI WA MBELE KUWASAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO IFAKARA -MOROGORO
March
2026
Wananchi wa kata za Kibaoni, Michenga, Lumemo na Lipangalala katika Halmashauri ya mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero, Mkoani Morogoro, wamelishukuru Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuwapatia msaada wa tani kumi za unga, unaolenga angalau kupunguza maumivu, kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha Machi 24 na 25, 2026.
Msaada huo umepokelewa na mbunge wa jimbo la Kilombero. Mheshimiwa Abubakari Asenga, mbele ya wananchi wa kata hizo katika hafla fupi iliyofanyika kijiji cha kibaoni, kata ya kibaoni, Halmashauri ya mji wa Ifakara, Mkoani Morogoro.
Akizungumzia msaada huo, Mheshimiwa Asenga, alisema analishuru Shirika la Reli Tanzania kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi wa Ifakara na kuyasihi makampuni na mashirika mengine kuiga mfano huo.
"Shirika letu la Reli limeonesha mfano mzuri sana, hiki walichokitoa ni kikubwa saana na wananchi wa Ifakara wamepokea kwa mikono miwili, niendelee kutoa rai kwa mashirika mengine ya serikali yajitoe tuweze kuwasaidia wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko" Alisema Mhe.Asenga.
Nae Bi.Magret James mkazi wa Ifakara amesema msaada huo unaaashiria mahusiano mazuri kati ya TRC na wananchi ambao ndio watumiaji na walinzi wakubwa wa huduma na miundombinu ya TRC .
Bwana Januari Haule ameongeza kuwa wananchi wa Ifakara wataendelea kutoa ushirikiano kwa TRC katika kuilinda miundombinu ya reli na kutokomeza vitendo vya wizi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano cha TRC, Bw. Fredy Mwanjala, alisema "tumeguswa na hali iliyowakumba wananchi wenzetu wa Jimbo la Kilombero kufuatia mafuriko aidha, kwa niaba ya Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TRC na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Machibya Shiwa, TRC inatoa msaada wa tani 10 za unga zenye thamani ya shilingi milioni 16, ili kusaidia kupunguza makali ya hali hii" alisema Mwanjala.
Aidha alisema, TRC inaelewa kuwa msaada huo hauondoi maumivu yote, lakini ni ishara ya mshikamano wa taasisi na wana Kilombero na kwamba iko karibu na wananchi katika nyakati zote ikiwemo nyakati hizi
Mvua iliyonyesha usiku wa Machi 24 na 25, 2026, ilisababisha pia kukatika kwa barabara kuu ya Ifakara- Mlimba katika maeneo ya Chita, Mbingu na Chage.
__________________________

