Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC KUWEKA MAGETI KWENYE UZIO WA RELI YA SGR


news title here
10
May
2024

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la kutoa uhamasishaji kwa viongozi wa mitaa kwenye maeneo mbalimbali yaliyopitiwa na mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR katika kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro linalofanyika Mei, 2024.

Zoezi la uhamasishaji linaambatanisha uwekaji wa mageti kwenye uzio ambao upo pembezoni mwa reli ya SGR ili kufanya maandalizi ya uendeshaji wa treni ya SGR ifikapo Julai, ambapo hapo awali uzio uliwekewa sehemu za wazi kwaajili ya kuruhusu wananchi kupita na kutumia njia ya mradi katika shughuli zao.

Meneja mradi msaidizi kipande cha kwanza kutoka TRC Mhandisi David Msusa ameeleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuweka mazingira ya kiusalama kwa binadamu na wanyama kwa kuzuia kukatiza katika njia hiyo ya SGR ili kuepusha maafa.

“Takwa moja la kuanza uendeshaji wa SGR ni lazima kuweka uzio ili kuepusha watu kukatiza na kuzuia uharibifu katika miundombinu ya reli” alisema Mhadisi Msusa.

Mhadisi Msusa alisema kuwa njia ya mradi ambayo imekua msaada mkubwa wananchi kufika katika maeneo mbalimbali kiurahisi hivyo TRC kushirikiana na TARURA watahakikisha wananchi wamepata njia mbadala ili kuweka wepesi kwa wananchi katika kuendelea kufanya shughuli zao za kila siku.

“Tumeanzia kutoa taarifa katika ngazi ya Mkoa wa Morogoro, ngazi ya Wilaya pamoja na kukaa kikao na wenzetu wa TARURA kuangalia njia mbadala ambazo zitaweza kutumika” alieleza Mhadisi Msusa.

Mhandisi Msusa alitaja maeneo yalioathiriwa katika wilaya ya Morogoro Mjini ni pamoja na mtaa wa Lukobe, Kilimanjaro, Yespa, Kihonda Kaskazini, Azimio, Tushikamane, Msimamo, Tungi, Seminari, Mikese, Tenki la Maji, Mtego wa Simba, Pangawe na Mkambarani.

Mwenyekiti wa mtaa wa Tungi Bw. Festo Faustin alisema kuwa uwekaji huo wa mageti kwenye uzio wa SGR utazuia athari hasa za watoto kwenda kuchezea miundombinu ya umeme na reli lakini pia amesisita TRC pamoja na TARURA kuhakikisha njia mbadala zinapatikana na kutengenezwa ili wananchi kutopata shida ya kusafiri kwa umbali mrefu kutafuta njia.

“Njia ya mradi ya SGR ndio ilikua mkombozi wa wananchi na kutumika kiurahisi kwa watoto kwenda mashuleni, kwenda kwenye vituo vya afya na maeneo mbalimbali hivyo njia mbadala zizingatiwe kwa kina na kwa haraka” alisema Bw. Koswa.

TRC inatarajia kuanza uendeshaji wa treni kupitia mradi wa SGR ambapo njia hiyo ya reli imewekwa uzio katika vipande vyote ambavyo mradi unapita kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza ili kuzuia ajali na hujuma katika miundombinu ya reli.