Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA ZAMBIA KUPITIA USAFIRISHAJI WA NJIA YA RELI


news title here
02
August
2022

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema amefanya ziara nchini Tanzania na kupata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro katika Stesheni ya reli ya kisasa jijini Dar es Salaam Agosti 02, 2022.

Rais wa Zambia amefanya ziara nchini Tanzania ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuingia madarakani ambapo lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili ambapo alitembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR ambayo itaunganisha nchi hizo kupitia biashara na usafirishaji.

Rais Hichilema akiambatana na wenyeji wake ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Liberata Mulamula, Dkt. Ally Possi Naibu Katibu Mkuu - Uchukuzi, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania - TRC Prof. John Kondoro, Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na Menejimenti ya TRC alipata taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa reli ya Kisasa na kushuhudia jengo la stesheni ya SGR Dar es Salaam na fursa za uwekezaji ndani ya stesheni.

Akiongea kwa niaba ya Rais Hichilema wakati wa ziara hiyo, Waziri wa Uchukuzi nchini Zambia Mhe. Franka Tayali amesema Serikali ya Tanzania imefanya jambo jema kujenga reli ya Kisasa ambapo kupitia ujenzi huu nchi ya Zambia itapata fursa ya kushirikiana kibiashara na nchi ya Tanzania kwa ukaribu na wepesi ukilinganisha na hapo awali. Ziara ya Rais wa zambia kutembelea ujenzi wa reli ya kisasa inaenda kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa reli nchini Zambia kwakuwa kila jema lifanyikalo Tanzania ni jambo jema kwa Zambia.

“Mheshimiwa Rais ni dhahiri kuwa kila jambo jema lifanyikalo Tanzania ni jambo jema pia kwa Zambia, ujenzi wa Reli ya Kisasa ni jambo ambalo limekuwa na mjadala katika bunge letu kwamba tunahitaji mapinduzi katika sekta ya usafiri wa Reli. hivyo basi katika ziara hii nimefanya juhudu za kusudi ili raisi aweze kufika hapa na kujionea kazi nzuri iliofanyika katika ujenzi huu” Alisema Mhemiwa Frank Tayali.

Aidha, Mheshimiwa Tayali ameongeza kuwa ujenzi wa SGR Tanania umeleta chachu katika kufikiria upya mapinduzi ya sekta ya usafiri wa reli nchini Zambia kwani tayari mikakati ya kujenga reli ya kisasa nchini Zambia imeeanza na baadhi ya mazungumzo ya awali na mkandarasi anayejenga reli hiyo nchini Tanzania YAPI MERKEZI imeeanza ili kufanikisha azma hiyo ya mapinduzi.

“Ujenzi huu wa SGR umetuhamasisha sana Zambia, tutakavyorudi nyumbani tutaendelea kufanya kazi na Tanzania kwa karibu sana na tutachukua hatua madhubuti ili kile ambacho kimefanyika Tanzania kiweze kufanyika Zambia, nina uhakika kwamba ujenzi wa SGR utatuunganisha na kutimiza matakwa ya Wazambia” alisema Mheshimiwa Waziri Tayali

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro ameeleza kuwa lengo la ujenzi wa reli ya kisasa ni kusaidia pia nchi za karibu za Afrika ili kuweza kusafirisha mizigo, hata hivyo Prof. Kondoro alisisitiza umuhimu wa kutembeleana na kuendeleza uhusiano wa karibu kwa maslahi ya maendeleo ya nchi za Afrika.

“Hatuwezi kufanya biashara kwa ufanisi na uwekezaji imara kama hakuna mahusiano ya karibu na nchi zinazotuzunguka ikiwa ni pamoja na Zambia, Kongo (DRC), Burundi na nchi zingine za Afrika, hivyo ziara ya Mhe. Rais Hichilema itadumisha uhusiano wetu hasa kibiashara“ alisema Prof. Kondoro.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa amesema Tanzania inashirikiana na Zambia kwa ukaribu katika sekta ya biashara pamoja na nchi jirani, Kadogosa aliongeza kuwa, Zambia inatumia bandari ya Dar es Salaam na kuna ushirikiano mkubwa katika reli ya TAZARA.

“Kwa mwaka huu hadi Juni Zambia wamepitisha tani milioni mbili na zaidi katika bandari ya Dar es Salaam na tunaingiliana Zambia kwa kupitia barabara kwa uelekeo wa Lubumbashi” alisema Kadogosa.

Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa kuna sababu kubwa kwa TRC kurudisha muunganiko wa Zambia na reli ya TAZARA kupitia reli ya kati TRC katika stesheni ya Kidatu, Mikumi ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Zambia.