Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC, CLOUDS MEDIA GROUP KUSAFIRISHA MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA KUELEKEA MKOANI KIGOMA


news title here
19
July
2021

Shirika la Reli Tanzania - TRC kwa kushirikiana na kampuni ya Clouds Media Group wameandaa treni maalumu itakayobeba mashabiki wa mpira wa miguu kuelekea mkoani Kigoma kutazama mechi kati ya Simba na Yanga itakayochezwa katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani humo siku ya Jumaapili Julai 25, 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ametoa tamko rasmi juu ya safari hiyo wakishirikiana na kampuni ya Clouds Media Group kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TRC, hivi karibuni Julai 19, 2021.

Ndugu Kadogosa amesema kuwa treni inatarajiwa kuanza safari katika stesheni ya Dar es Salaam kuelekea Kigoma siku ya Ijumaa Julai 23, 2021 na kufika Kigoma siku ya Jumamosi Julai 24, 2021 na baadae treni hiyo itaanza safari kurudi Dar es Salaam siku hiyo ya Jumapili Julai 25, 2021 majira ya saa 03.00 usiku mara baada ya mechi kuisha.

Aidha Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa tiketi zitapatikana katika stesheni za Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Manyoni, Tabora na Kigoma pia tiketi zitapatikana kwa njia ya mtandao ambapo zitapatikana kwa mashabiki na wananchi wote ili kuweza kusafiri katika treni aina ya Deluxe ambayo itakua na behewa 14 zenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 800.

“Gharama za usafiri ni kwa madaraja, daraja la tatu kukaa ni TZS. 100,000/= na daraja la pili kukaa ni TZS. 120,000/= na daraja la pili kulala ni TZS. 150,000/= kwenda na kurudi kwa gharama hiyo hiyo , alisema Ndugu Kadogosa”.

Vilevile Ndugu Kadogosa amewaasa mashabiki na wananchi wote waendelee kujikinga na janga kubwa la ugonjwa wa korona kwa kutumia vitakasa mikono pindi wakiwa safarini pamoja na kila mtu kujilinda na mikusanyiko.

Naye Mkuu wa Mikakati na Ubunifu kutoka kampuni ya Clouds Media Group Bw. Ruben Ndege amesema kuwa ndani ya safari hiyo kutakua na burudani za aina mbalimbali za mziki , wasanii akiwemo msanii wa mziki wa kizazi kipya Saidi Chege Chigunda, pamoja na michezo mbalimbali ya gemu, bao , drati, karata. Chakula pamoja na vinywaji mbalimbali.

“Kazi yetu kama Clouds Media Group ni kutoa nafasi kwa vijana wanaopenda burudani, alisema Bw. Ndege”.

Hata hivyo TRC kwa kushirikiana na Clouds Media Group wametoa fursa kwa wadau wote waliotayari kudhamini safari hiyo ili kuwapatia nafasi ya kujitangaza ndani ya treni pamoja na kujitangaza katika stesheni kubwa zote zilizopo njia ya kuelekea kigoma na kuweza kupata matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni na redio ya clouds .