TEKNOLOJIA KATIKA MRADI WA SGR ZAWAVUTIA WAJUMBE WA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA WADAU WA USAFIRISHAJI

April
2021
Wajumbe wa kongamano la kimataifa la wadau wa miundombinu ya usafirishaji kutoka nchi mbalimbali duniani, wametembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR kuanzia Dar Es Salaam hadi Kilosa mkoani Morogoro, Aprili 29, 2021.
Wajumbe wa kongamano hilo la siku mbili lililofanyika katika kituo cha Kimataifa cha mikutano cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya namna ambavyo teknolojia za kisasa zinaweza kutumika kuendeleza miundombinu ya uchukuzi, wametembelea Stesheni ya SGR ya Dar es Salaam, kituo cha Kupoozea umeme kilichopo umbali wa KM 26 kutoka Dar es Salaam, Karakana ya Treni za Kisasa eneo la Kwala mkoani Pwani na handaki namba mbili la reli ya kisasa ya SGR, Kilosa Mkoani Morogoro.
Kiongozi wa msafara wa wajumbe hao Bw. Bruno Kinyaga, ameeleza kuwa lengo kutembelea mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa limetokana na ukweli kuwa Reli hii ni moja ya Miundombinu ya kisasa nchini na eneo zima la Afrika Mashariki na kati vilevile matumizi ya mifumo ya teknolojia za kisasa katika reli ya SGR yanaenda sambamba na lengo la Kongamano lao.
“Tumekuja hapa kujifunza kwa vitendo, lakini pia kama wataalamu katika sekta ya uchukuzi tunatazama pia namna gani tunaweza kushauri kwa lengo la kuboresha zaidi miundombinu hii” aliongeza Bw. Kinyaga.
Kwa upande wake mwenyeji wa msafara wa wajumbe hao, Mkurugenzi wa Miundombinu na Ujenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Mhandisi Faustin Kataraia, ameeleza kuwa ziara hiyo ina faida kubwa kwa Shirika na Mradi, kwani mada kuu ya Kongamano la wadau hao inakwenda sambamba na dhamira kubwa ya kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri kwa njia ya Reli, kupitia Reli ya Kisasa ya SGR itakayotumia nishati ya umeme, hivyo maoni na ushauri wa wadau hao utasaidia katika ujenzi wa mradi huo wa kihistoria unaoendelea nchini.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa Kongamano hilo lililoshirikisha mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya bara la Afrika wakiwa katika ziara ya kutembelea mradi wa SGR hawakusita kuelezea namna mradi huo unavyotazamwa kama mfano mkubwa kwa nchi za bara la Afrika hasa kwakuwa unatekelezwa kwa fedha za ndani.
“Kwanza kabisa huu ni mradi mkubwa, kwa hakika tunavutiwa na kile ambacho Tanzania inafanya, huu ni uwekezaji mkubwa unaolenga maendeleo, kazi iliyofanyika hakika haielezeki, si mara zote utafanya maendeleo kwa fedha za wahisani, tunatakiwa kuwa na rasilimali zetu za ndani, hivyo jambo moja la kuupongeza uongozi kwa kazi hii ni kwamba kupitia kazi hii wanaandika historia mpya ya uongozi Afrika, kwa sababu mara zote tumekuwa tukitazamwa kama tulioshindwa kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha za umma” alieleza Bw. Clifford Gobo, mjumbe kutoka Zimbabwe.
Ziara hii inafanyika wakati ambapo shughuli za ujenzi katika vipande hivyo viwili zikiendelea vizuri ambapo kipande cha kwanza cha Dar es Salaam hadi Morogoro kikiwa na zaidi ya 91% huku kikitegemewa kufikia hatua ya majaribio ya treni za kisasa zinazotumia umeme mapema mwezi Agosti, 2021.
Aidha, katika kipande cha pili cha mradi kuanzia Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida, ujenzi umefikia 58% ikiwa ni zaidi ya nusu ya kazi, ujenzi wa tuta tu katika kipande hiki ukifikia zaidi ya 70%, na Reli ikiwa imekwishatandikwa kuanzia Morogoro mpaka Kilosa ambazo ni takribani KM 74 huku Reli ikiwa imekwisha tandikwa kuanzia Ihumwa mpaka Mpwapwa mkoani Dodoma.