Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TCB KUJIONEA FURSA ZILIZOPO KATIKA MRADI WA SGR


news title here
27
August
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea kufanya ziara na menejimenti kutoka benki ya TCB kutembelea mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro na kipande cha pili Morogoro - Makutupora iliyofanyika hivi karibuni Agosti, 2022.

Ziara hiyo ya menejimenti ya benki ya TCB imejikita katika kuona fursa mbalimbali za uwekezaji wa kibiashara zipatikanazo katika maeneo ya mradi wa SGR ikiwemo kwenye stesheni kuu za SGR na stesheni ndogo.

Mwenyekiti wa Bodi ya TRC Profesa John Kondoro alisema kuwa mradi wa SGR ni mradi mkubwa ambao uko mbioni kuanza shughuli za uendeshaji ambapo wawekezaji watapata fursa za kufanya biashara pamoja na maeneo mazuri yatakayotumika kama utalii wa ndani.

“Mtazamo wa reli sio kusafirisha pekee, pia tunatengeneza maeneo ambayo watu wanaweza kupata fursa mbalimbali hivyo tunashukuru TCB kuja kuona fursa zilipo“ alisema Prof. Kondoro.

Profesa Kondoro aliongeza kuwa wananchi watakuwa na uhitaji mkubwa wa kufanya miamala ya kifedha katika safari na kwenye kusafirisha mizigo hivyo fursa za kuwa na huduma za kibenki katika stesheni za SGR ni moja ya fursa muhimu itakayorahisisha mahitaji ya kifedha kwa abiria kuwa na wepesi.

“Dunia ya leo teknologia imebadilika hivyo ni lazima twende kisasa” alisema Prof. Kondoro.

Naye Mwenyekiti wa Bodi kutoka benki ya TCB Dkt. Edmund Mndolwa ameeleza kuwa amejifunza mambo mengi kupitia ziara hiyo na kuona fursa watakazozipata ikiwemo kuweka matawi pamoja na mashine za kutolea fedha (ATM ) ili kuweza kurahisisha huduma kwa wananchi.

“TCB lazima tuwe wa kwanza kuweka matawi yetu katika stesheni za SGR, huu mradi utafanya mzunguko wa biashara kuwa mkubwa “ alisema Dkt. Mndolwa.

Pia Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka TCB Bw. Jema Msuya alisema kuwa miundombinu inachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uchumi wa nchi kwa kuleta fursa mbalimbali kwa wawekezaji hivyo ni jambo muhimu TCB kuwa moja ya mdau atakaefanya uwekezaji katika mradi huo wa kimkakati wa SGR.

“Eneo la Kwala ni moja ya sehemu zenye fursa kubwa kwa kuwa ni sehemu kubwa ambayo mizigo mingi itashushwa na wafanyabiashara kuja kwa wingi” alisema Bw. Msuya.

Hata hivyo Bw. Msuya alieleza kuwa ushirikiano wa taasisi za kifedha na serikali ni kuhakikisha kufanya kazi kwa ukaribu katika kuchangia huduma za kifedha kwaajili ya manunuzi mbalimbali ikiwemo manunuzi ya vifaa.

“Lazima tuhakikishe kunakuwa na nguvu ya ndani katika nchi” alisema Bw. Msuya.

Benki ya TCB inatarajia kufanya ziara hiyo na kuendelea kuangalia fursa mbalimbali katika mradi hadi kwenye kipande cha tano cha mradi wa SGR Isaka - Mwanza.