Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TANZANIA YAWAFUNDA WAZAMBIA KUHUSU SGR


news title here
26
May
2025

Kamati ya Bunge ya Utawala wa Mitaa, Makazi na Masuala ya Machifu kutoka nchini Zambia, imelitembelea Shirika la Reli Tanzania hususani Stesheni ya Magufuli Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Reli ya SGR na kujifunza namna ujenzi huo ulivyotekelezwa kwa usainifu wa hali ya juu ikiwemo pia kuzitambua fursa za uwekezaji zinazopatikana kupitia mradi wa SGR na kujionea uendeshaji wake.

Akiongea wakati wa ziara hiyo ya Mei 23, 2025 Mwenyekiti wa Kamati hiyo inayojumuisha wabunge 11 Mhe. Twaambo Mwitinta, amesema kuwa kupitia ziara hiyo wameweza kufahamu vyema ujenzi wa mradi wa reli ya SGR aidha kujifunza umuhimu wa sekta ya reli katika kukuza uchumi na kuboresha mawasiliano ndani na nje ya nchi kwa ujumla.

"Tumefanya maamuzi mazuri sana kuja kutembelea SGR, tumeweza kufahamu kwa undani zaidi namna TRC imefanya na inaendelea kufanya kazi katika kuhakikisha inaboresha sekta ya uchukuzi na mawasiliano kupitia ujenzi wa reli hii na huduma zake hasa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati" Amesema Mhe. Mwitinta.

Aidha, Mhe. Twaambo amewasihi wananchi Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha miradi iliojengwa kwa uwekezaji mkubwa inalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Senzige Kisenge, amesema kutokana na ziara ya Wabunge wa Zambia na TRC wamejifunza mambo mbalimbali ya kiutendaji haswa katika shughuli za uendeshaji wa treni za SGR na kubadilishana uzoefu unaolenga kuboresha huduma na shirika kwa ujumla.

"Kusema ukweli ujio huu unamaana kubwa sana haswa katika kubadilishana uzoefu na pia wametupa mawazo jinsi ya kuboresha huduma zetu nakadhalika na kwa ujumla tumebadilishana mawazo na uzoefu katika utendaji" Amesema Mhandisi Senzige.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea kufungua milango katika nchi za Afrika zinazo tamani kujifunza na kufahamu teknolojia na utaalamu uliotumika katika ujenzi wa reli ya SGR.