Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TANZANIA NA ITALIA ZASAINI MOU KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KISASA KATIKA SEKTA YA RELI


news title here
07
August
2026

Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Prof. Makame M. Mbarawa (Mb), alifanya ziara rasmi nchini Italia kufuatia mwaliko wa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia. Ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano wa kiufundi kati ya Tanzania na Italia kupitia shughuli kuu tatu; kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), FS Engineering S.p.A. na ITS Engineering S.r.l., kujionea matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa miundombinu ya reli, pamoja na kutembelea miradi ya kimkakati inayosimamiwa na FS Engineering ili kujifunza mbinu bora za usimamizi wa miradi mikubwa ya miundombinu.

Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Mheshimiwa Waziri ulijumuisha viongozi na wataalamu kutoka TRC waliopata fursa ya kujifunza mifumo ya kisasa inayotumika nchini Italia katika kubuni, kupanga, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya miundombinu kwa kutumia teknolojia za kidijitali.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa pamoja na Naibu Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia, Bw. Edoardo Rixi, aliyemwakilisha Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia, walishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya M. Shiwa, kwa niaba ya Shirika la Reli Tanzania, Dario Lo Bosco kwa niaba ya FS Engineering S.p.A. na Michele Titton kwa niaba ya ITS Engineering S.r.l.

FS Engineering ni kampuni tanzu ya Ferrovie dello Stato Italiane (FS Group), shirika la kitaifa la reli la Italia, iliyoanzishwa kutoa huduma za ushauri wa kihandisi, usanifu, usimamizi wa miradi na usimamizi wa ujenzi wa miradi ya miundombinu ya reli na sekta nyingine za usafiri. Kampuni hiyo inatumia teknolojia za kisasa za kidijitali katika kubuni, kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi, na imekuwa mshauri wa miradi mbalimbali ya kimkakati ndani na nje ya Italia. Aidha, ITS Engineering inakamilisha ushirikiano huo kupitia utaalamu wake katika uhandisi wa miundombinu, mazingira na ujenzi.

Makubaliano hayo yanaweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo katika kubadilishana utaalamu wa kihandisi, kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kujenga uwezo wa wataalamu wa TRC kupitia mafunzo na programu za maendeleo ya kitaalamu, pamoja na kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kubuni, kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya reli.

Aidha, ushirikiano huo unalenga kuimarisha uwezo wa TRC katika kubuni miradi mipya ya reli, kuboresha mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa miundombinu, kuimarisha huduma za ushauri wa kihandisi, kuongeza ufanisi wa biashara ya reli na kuendeleza suluhisho bunifu zitakazochangia reli kuwa endelevu, yenye tija na inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya uchukuzi nchini.

Katika kuendelea na ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania ulitembelea Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Uendeshaji wa Reli (National Control Room) cha Rete Ferroviaria Italiana (RFI), ambacho kinasimamia uendeshaji wa mtandao wa reli nchini Italia kwa wakati halisi kupitia mfumo unaounganisha vituo vya udhibiti vya kikanda.

Ujumbe ulijifunza namna kituo hicho kinavyoratibu uendeshaji wa treni za abiria na mizigo, kusimamia mtiririko wa trafiki ya reli, kuratibu shughuli za matengenezo ya miundombinu na kushughulikia changamoto mbalimbali za kiutendaji ili kuhakikisha usalama, ufanisi na mwendelezo wa huduma za reli katika mtandao mzima wa nchi. Aidha, ilielezwa kuwa upangaji wa matengenezo ya miundombinu hufanyika kwa muda mrefu na kuratibiwa kwa karibu na idara za uendeshaji, biashara na udhibiti wa trafiki ili kupunguza athari kwa huduma za usafiri na kuhakikisha matumizi bora ya miundombinu.

Baada ya ziara katika Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Uendeshaji wa Reli, ujumbe ulielekea jijini Florence, ambapo ulitembelea moja ya miradi mikubwa ya miundombinu inayosimamiwa na FS Engineering.

Katika mradi huo, wataalamu wa FS Engineering walionesha namna teknolojia za kisasa zinavyotumika katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi kuanzia usanifu, upangaji, usimamizi wa ujenzi hadi ukaguzi wa ubora wa kazi. Ujumbe ulipata fursa ya kujionea matumizi ya Building Information Modelling (BIM), LiDAR Survey, kamera zenye Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) pamoja na Digital Control Room, ambapo taarifa kutoka eneo la mradi hukusanywa, kuchambuliwa na kuwasilishwa kwa wakati halisi ili kusaidia usimamizi wa mradi.

Teknolojia hizo huwezesha kufuatilia maendeleo ya kazi za wakandarasi, kutathmini ubora wa kazi zinazotekelezwa, kubaini mapema changamoto zinazoweza kuathiri mradi, kufuatilia utekelezaji wa mikataba kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali. Mfumo huo pia husaidia kufanya maamuzi yanayotokana na taarifa sahihi na za wakati halisi, hivyo kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu.

Aidha, ujumbe wa Tanzania ulifanya majadiliano ya kiufundi na wataalamu wa FS Engineering kuhusu mbinu bora za usimamizi wa miradi, matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi na namna mifumo hiyo inaweza kutumika kuimarisha usimamizi wa miradi ya reli nchini Tanzania.

Ziara hiyo imefungua fursa mpya za ushirikiano wa kiufundi kati ya Tanzania na Italia katika sekta ya reli. Kupitia sekta ya reli, Hati ya Makubaliano iliyosainiwa itaiwezesha TRC kunufaika na uhamishaji wa teknolojia za kisasa, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, kujengewa uwezo wa wataalamu wake, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi ya reli kwa kutumia mbinu na teknolojia za kisasa. Aidha, ushirikiano huo unakuja wakati TRC ikiendelea kuimarisha huduma zake za ushauri wa kihandisi kupitia kitengo chake cha Engineering Consultancy, hivyo kufungua fursa za kushirikiana na taasisi zenye uzoefu wa kimataifa katika kubuni, kusimamia na kutekeleza miradi ya miundombinu ya reli.

Hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuendelea kuimarisha sekta ya reli kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza uwezo wa kitaalamu wa watumishi, kuboresha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya reli, kuongeza ujuzi na ufanisi katika usimamizi na uendeshaji, kuhakikisha uendelevu wa miundombinu ya reli (sustainability), na kuongeza mchango wa sekta ya reli katika maendeleo ya uchumi wa Taifa pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.