Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TANZANIA, BURUNDI NA JAMHURI YA DEMOKRASIA YA KONGO KUJENGA RELI YA KISASA PAMOJA


news title here
02
February
2020

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Tanzania Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo Mhe. Didier Mazenga Mukanzu watembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR jijini Dar es Salaam, Januari 2020.

Lengo la ziara ya Mawaziri wa nchi hizo mbili ni kuhakikisha maagizo ya Marais wa nchi za Tanzania, Burundi na Kongo ya kujenga reli ya kisasa kuanzia Uvinza – Msongati hadi Kongo yanatekelezwa kikamilifu ili mizigo ya Kongo na Burundi inayoingia katika Bandari ya Dar es Salaam iweze kusafirishwa kwa haraka na kwa bei nafuu, lakini pia kurahisisha muingiliano wa kibiashara katika nchi hizo.

Katika kutekeleza maagizo hayo tayari Tanzania na Burundi imekamilisha upembuzi na usanifu wa reli ya kisasa kutoka Uvinza Tanzania hadi Msongati Burundi ambapo nchi hizo mbili ziliamua kuchanga fedha ili kumuajiri Mhandisi Muelekezi aweze kufanya kazi ya usanifu wa reli hiyo, lakini katika hatua nyingine nchi za Kongo na Burundi zimekubaliana kuchanga fedha ili ziweze kufanya upembuzi na usanifu wa reli kutoka Msongati hadi Kongo kabla ya taratibu za kutafuta mkandarasi wa ujenzi wa reli hiyo kuanza.

“Mkutano wa kwanza tulifanya Kigoma, mkutano wa pili tulifanya Bujumbura na mkutano wa tatu tutafanya Lubumbashi mwezi wa tatu mwishoni 2020, maendeleo yaliyofikiwa mpaka hivi sasa kwa upande wa reli ya kutoka Uvinza mpaka Msongati usanifu umekamilika na usanifu huo tulichanga fedha kati ya Tanzania na Rwanda, kwenye mkutano wa juzi Burundi na Kongo wamekubaliana kuchanga fedha ili wafanye usanifu kutoka Msongati – Uvira hadi Kongo” alisema Waziri Kamwelwe

Mradi huu utakuwa ni wa pamoja kati ya Tanzania, Burundi na Kongo kutoka Uvinza – Msongati – Kongo, malengo ya mradi huu ni kupunguza gharama za usafirishaji kati ya nchi hizi tatu, kutokana na hilo tayari Serikali ya Tanzania imejenga Bandari kavu ya Katosho mkoani Kigoma ili Mabehewa yanayofika Bandari ya Dar es Salaam yawe yanapakiwa na kwenda kushushwa Katosho Kigoma

Naye Waziri wa Uchukuzi Kongo amemshukuru Waziri Kamwelwe, ameongeza kuwa ameweza kuona Mradi wa reli ya kisasa ambao umemfurahisha sambamba na Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mukanzu amesema kuwa anaihakikishia Mamlaka ya Bandari kuwa mradi wa reli kati ya Tanzania, Burundi na Kongo utakapokamilika biashara itakua kwa sababu mizigo itaweza kupitia Ziwa Tanganyika na mizigo mingine itapita kwenye reli mpaka Kongo

“Sisi mawaziri tunawakilisha nchi zetu na Marais wetu walivyokubaliana ya kwamba ni vizuri wajenge reli itakayounganisha nchi hizi tatu” alisema Waziri Mukanzu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameshukuru ujio wa mawaziri hao kuona mradi wa reli ya kisasa na Bandari ambavyo kwa pamoja vinashirikiana katika kuhakikisha mzigo unasafirishwa kwa gharama nafuu na kupunguza bei za bidhaa kwa walaji

“Tunawashukuru sana Mawaziri wetu wa uchukuzi kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari na Shirika la Reli kuona ujenzi wa reli, tukiimarisha usafiri wa reli hata gharama za usafirishaji na bidhaa zitashuka sana na hilo ndio lengo kuu” alisema Kadogosa

Halikadhalika Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Mhandisi Deusdedith Kakoko amesema kuwa ziara ya Waziri huyo imeleta matumaini makubwa kwa kuwa ameona mradi wa reli ya kisasa unaoendelea lakini pia Bandari ya Dar es Salaam ambayo inafanya kazi kubwa ya kupitisha mizigo mingi inayoelekea nchini Kongo

“DRC hasa kuanzia mwaka jana ndio nchi inayoongoza kupitisha mizigo yake katika Bandari ya Dar es Salaam ikifuatiwa na Zambia, hivyo ujio huu unazidi kutuongezea matumaini kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameweza kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itajengwa hadi nchini Kongo pamoja na Bandari ya Dar es Salaam ambayo itakuwa ikipokea mzigo kwa ajili ya kusafirishwa na reli hiyo” alisema Mhandisi Kakoko