Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKATABA WA UJENZI WA RELI YA KISASA AWAMU YA PILI KUTOKA MOROGORO HADI MAKUTUPORA WASAINIWA


news title here
09
May
2018

Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO) imeingia mkataba na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kujenga kipande cha pili cha reli ya kisasa(SGR) kutoka Morogoro hadi Makutopora yenye urefu wa kilomita 336 za njia kuu na kilomita 86 za njia za kupishana treni na maeneo ya kupangia mabehewa jumla kilomita 422 kwa uzani wa tani 35 kwa ekseli.

Kandarasi hii itakuwa na thamani ya jumla TShs. Trilioni 4.3., mkataba umetiwa saini na Mtendaji Mkuu wa RAHCO na TRL Ndg. Masanja Kadogosa na Mwanasheria wake Ndg. Petro Mnyeshi na kwa upande wa Yapi Merkezi waliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Bodi wake Bwana Erdem na Mkuu wa Miradi ya Ethiopia na Tanzania Bwana Abdullah.

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amesema utiaji sahihi wa kandarasi hii ya pili ni kuonesha dhamira isotetereka ya Serikali ya awamu ya 5 kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya reli nchini kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Amesema reli ya kisasa(SGR) italeta mabadiliko makubwa sana kiuchumi na kijamii na maendeleo kwa jumla. Kwanza zitaokoa uharibifu wa barabara zilizojengwa kwa gharama kubwa. Bidhaa zinazosafirishwa kwa masafa marefu zitafika kwa gharama ndogo hivyo walaji watazinunua kwa bei nafuu.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Ruaha katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(JKNICC) ilihudhuriwa na kaimu balozi wa Uturuki nchini pamoja na Wawakiishi wa Kampuni ya Yapi Merkezi.

Wengine waliohudhuria ni Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakiongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho.

Mapema mwaka huu Februari 03, 2017, Yapi Merkezi na Mota Engil ya Ureno ziliingia mkataba na RAHCO wa kujenga kipande cha kwanza cha reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro urefu wa jumla wa Kilomita 303. Ujenzi wa kipande hicho ulitiwa jiwe la msingi na Rais wa Tanzania Dk John Magufuli hapo Aprili 12, 2017 katika hafla kubwa ya aina yake iliyofanyika katika kituo cha Reli cha Pugu nje ya jiji la Dar es salaam.