SIMBA KUTUA NA SGR MOROGORO
July
2024
Kilabu ya Mpira wa Miguu ya Simba imeingia makubaliano na Shirika la Reli Tanzania – TRC kwaajili ya kutumia usafiri wa treni ya reli ya kiwango cha kimataifa - SGR katika Stesheni ya SGR ya Tanzanite jijini Dar es Salaam Julai 22, 2024.
Lengo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani katika ujenzi wa mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa, safari za Dar es Salaam na Morogoro zimeanza ambapo Julai 25, 2024 safari za Dar es Salaam hadi Dodoma zitaanza rasmi.
Aidha, Klabu ya Simba itatumia usafiri wa SGR ambao ni rahisi na wa haraka zaidi kuelekea Mkoani Morogoro Julai 24, 2024 kwenye Uzinduzi wa Sherehe za Wiki ya Mashabiki na Wapenzi wa Kilabu ya Simba.
Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Siimba ameeleza kubwa uzinduzi wa Wiki ya Simba utafanyika mkoani Morogoro katika hifadhi ya Mikumi, Kilabu ya Simba itatumia muda mfupi kusafiri na treni ya SGR kwenda Morogoro na kurudi Dar es Salaam.
“Ni rahisi sana kwa wote kwenda Morogoro kwenye Uzinduzi wa Wiki ya Kilabu ya Simba, kusafiri kwa urahisi na haraka kwa muda wa dakika 90 na kufika mapema kufanya shughuli mabalimbali za matawi Morogoro” ameeleza Imani Kajura
Mkurugenzi Mkuu TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa huduma za SGR zinamuwezesha kila mtanzania kupanda treni za umeme kulingana na nauli rafiki zilizowekwa na Serikali, pia TRC inashirikiana vyema na Kilabu ya Simba kwenda na kurudi Morogoro kwa kutumia treni ya Umeme ya SGR katika uzinduzi wa Wiki ya Simba Mikumi Mkoani Morogoro
.
“Ni tukio la kizalendo kwa Simba kwa nchi yao kuchochea utalii wa ndani katika mbuga ya Mikumi pia SGR ndiyo inaanza tunahitaji kuitangaza sana, tunashukuru sana Simba kwa kutushirikisha kwenye tukio hili” Mkurugenzi Mkuu TRC amezungumza
Sanjari na hayo Msemaji Mkuu wa Klabu ya Simba aipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza katika Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa, Kilabu ya Simba itakuwa balozi mkubwa katika kuitangaza SGR.
“SGR ni bidhaa mpya iliyoingia Tanzania, Sisi kama Simba lazima tupige kelele kuwaambia Watanzania wasiuchukulie poa mradi uliowekezwa kwa maelfu ya fedha ni jambo kubwa ambalo limefanyika na lazima kuipongeza Serikali yetu kwa kuhakikisha mradi huu unasimama” amezungumza Ahmedi Ally
Kilabu ya Simba imepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa unatekelezwa kwa kusimamiwa vyema kabisa na Shirika la Reli Tanzania ikiwa ni moja ya malengo ya kutimiza utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi.