Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHULE YA MSINGI ITIGI RELI YAHAMASISHA SHULE NYINGINE KUTEMBELEA MRADI WA SGR ILI KUJIFUNZA ZAIDI


news title here
10
October
2020

Walimu na Wahitimu wa Elimu ya Msingi katika Shule ya Itigi Reli watembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kipande cha Morogoro – Makutupora ambapo mbali na kuona mradi huo wametoa rai kwa shule nyingine kutembelea mradi huo ili kujifunza zaidi, Oktoba 10, 2020.

Lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna mradi huo mkubwa unavyotekelezwa na kuwapa wanafunzi hamasa ya kuwa na uzalendo kwa kusoma kwa bidii ili waweze kuwa miongoni mwa wataalamu watakaosimamia mradi huo siku zijazo.

Ziara hiyo ilianzia katika Kambi ya Ujenzi SGR ya Ihumwa iliyopo jijini Dodoma ambapo wanafunzi na walimu walipata maelezo kutoka kwa wahandisi kuhusu utekelezaji wa mradi pamoja na maendeleo ya mradi huo ambao umefikia zaidi ya 43% kwa kipande cha Morogoro – Makutupora.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa alitoa ahadi katika Mahafali ya 27 ya Darasa la Saba katika Shule hiyo kwa ajili ya kuwapeleka wanafunzi wa Shule hiyo inayomilikwa na Shirika la Reli kutembelea Mradi wa SGR ili waweze kuona mapinduzi yanayofanyika katika sekta ya reli wakiwa kama wadau wakubwa wa reli.

Shule ya Msingi Itigi Reli ilianzishwa mwaka 1987 lengo likiwa ni kutoa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wa Shirika la Reli wanaofanya kazi katika maeneo ambayo hakuna shule za msingi au shule ziko mbali na maeneo wanayofanyia kazi, shule hii ilizinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi Aprili 04, 1993 ikiwa chini ya umiliki wa Shirika la Reli.

Mkuu wa Shule ya Itigi Reli Bi. Grace Gyunda ameeleza furaha yake kufuatia utekelezaji wa ahadi hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu TRC, pia Bi. Grace ametoa shukurani za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu na wafanyakazi waliowezesha ziara hiyo.

“Napenda kumshukuru Mkurugenzi Mkuu Bwana Masanja Kadogosa kwa kutupa fursa hii kutembelea mradi wa SGR, tumejifunza mambo mengi, wanafunzi walikuwa na hamu ya kuona kitu cha namna hii, tuliongea kama utani lakini yeye ni mtu wa vitendo tunamshukuru sana” alisema Bi. Grace

Bi. Grace aliongeza kuwa “Ukiwa mtaani huwezi kujua kazi kubwa inayofanyika, kazi ni kubwa sana inayofanyika naipongeza sana serikali ya awamu ya tano pia nashauri Wanafunzi na Walimu wa Shule nyingine waje wajifunze kwa sababu wanafunzi hawa ndio watakaokuwa wahandisi wa kesho na walinzi wa reli hii”

Halikadhalika Wanafunzi wa Shule ya Itigi Reli wameeleza furaha yao sambamba na mambo kadhaa waliyojifunza baada ya kutembelea sehemu mbalimbali katika mradi huo kuona kazi zinazofanyika,

“Nimefurahi kuja kuona mradi wa SGR, tunawashukuru watumishi kwa kutuleta huku kuona jinsi reli inavyojengwa” alisema Celina Juma, Mhitimu wa Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Itigi Reli

Naye Abdallah Jabu amemshukuru Rais Magufuli kwa juhudi anazofanya kujenga mradi huo mkubwa wenye manufaa, pia amewashauri wanafunzi wengine watembelee mradi huo ili waweze kuona na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa – SGR.

Shirika la Reli limekuwa likiendesha ziara za makundi mbalimbali ya watu kutoka sehemu tofauti ndani na nje ya nchi ili kuongeza ufahamu na uzoefu kuhusu masuala ya ujenzi wa reli kupitia miradi yake hususani mradi mpya na mkubwa wa SGR ambapo kupitia ziara hizo makundi ya watu tofauti yameweza kunufaika kwa kujifunza na kutambua fursa zilizpo katika mradi huo wa kimkakati.