Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHIRIKA LA RELI TANZANIA – TRC LAZINDUA CHAPISHO LA GAZETI LA RELI NA MATUKIO


news title here
31
January
2020

Wakati TRC ikiendelea na kampeni ya uelewa kuhusu kuzuia ajali na hujuma dhidi ya miundombinu ya reli, Leo hii Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania – TRC Prof. John Kondoro azindua chapisho la ‘GAZETI LA RELI NA MATUKIO’ toleo maalum la 2019 katika ukumbi wa mikutano ofisi ya makao makuu TRC jijini Dar es Salaam Januari 31, 2020.

Gazeti hilo limezinduliwa likiwa na lengo la kuelimisha umma na kutoa taarifa kuhusu huduma zinazotolewa pamoja na miradi ya kimkakati inayosimamiwa na kuratibiwa na Shirika la reli nchini ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa – SGR, uboreshaji na ufufuaji wa reli ya kati – TIRP na ukarabati wa mabehewa.

Kwa upande mwingine gazeti litatoa fursa kwa wadau mbalimbbali yakiwemo mashirika, kampuni na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi kutumia gazeti la reli kutangaza biashara na huduma wanazotoa kwa lengo la kutoa taarifa kwa jamii.

Hapo awali gazeti hili lilikua likitoka kwa njia ya mtandao pekee mara moja kwa mwezi kuelezea shughuli zinazoendelea na matukio ambayo hutokea katika majukumu ya kila siku ya TRC na kuwekwa katika tovuti ya shirika (www.trc.co.tz) na kusambazwa kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa jina la @tzrailways.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi amelipongeza Shirika kwa kuandaa gazeti ambalo litakuwa na mchango mkubwa kwa Shirika na Serikali hasa katika kutoa taarifa kwa umma hususani kuhusu miradi ambayo Serikali ya awamu ya tano inatekeleza kupitia Shirika la reli Tanzania. Aidha, Prof. Kondoro amesisitiza kuwa wananchi wanayo haki ya kupata taarifa hivyo Gazeti hili limekuja muda muafaka ambapo Shirika liko katika mabadiliko chanya kiutendaji hivyo umma utapata fursa ya kufahamu mengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa, ametoa wito kwa mashirika, kampuni na taasisi za Serikali na binafsi kutumia fursa ya gazeti la shirika reli kutangaza biashara zao na huduma wanazotoa, hivyo itasaidia huduma na bidhaa zao kujulikana kwa watu wengi kwa kuwa gazeti hilo litapatika mtandaoni lakini pia kwenye treni ambapo treni hubeba watu wengi, hivyo taarifa zao zitawafikia watu wengi kwa urahisi.