Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SHIRIKA LA RELI TANZANIA -TRC LACHANGIA UKARABATI WA BARABARA MOROGORO VIJIJINI


news title here
05
December
2020

Shirika la Reli Tanzania – TRC limetoa mchango wa ukarabati wa barabara Morogoro Vijijini katika tarafa ya Ngerengere hivi karibuni Disemba, 2020 ikiwa ni sehemu ya kuleta maendeleo katika jamii zilizopo jirani na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC Bi. Jamila Mbarouk akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TRC amesema kuwa Shirika limechangia kukarabati barabara hiyo kwa kuijenga katika kiwango cha changarawe kwa kushirikiana na Mkandarasi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa Yapi Merkezi.

Bi. Jamila amesema kuwa Shirika limefanikiwa kujenga Reli ya Kisasa kutokana na fedha na kodi za wananchi hivyo shirika halina budi kuwa karibu na jamii katika kusaidia na kutatua changamoto zilizopo ikiwemo ya barabara hiyo ambayo itanufaisha maisha ya wananchi.

“Barabara hii ya Morogoro Kusini Mashariki ina zaidi ya miaka 15 bila kukarabatiwa, hivyo ukarabati huu ukikamilika utarahisisha na kutatua changamoto za usafiri” alisema Bi. Jamila.

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamis Taletale ametoa shukrani za dhati kwa serikali ya awamu ya tano pamoja na TRC kwa kukubali ombi lake la kuikarabati barabara hiyo kwani itawasaidia wananchi katika mambo mengi ikiwemo kurahisisha usafiri ambapo italeta tija pia katika kupunguza gharama za maisha kwa wananchi katika maeneo hayo.

Vilevile Mhe. Taletale amewasisitiza wananchi Tarafa ya Ngerengere kulinda na kutunza miundombinu ya reli kwa kuwa miundombinu hiyo inajengwa kwa ajili ya wananchi na kuwarahisishia huduma za usafiri wa abiria pamoja na mizigo ambapo pia watapata fursa mbalimbali zikiwemo fursa za ajira pamoja na biashara.

“Maendeleo ya nchi yeyote yanatokana na kuwa na miundombinu bora ya reli pamoja na barabara” alisema Mhe. Taletale.

Hata hivyo, wananchi wa Tarafa hiyo ya Ngerengere wameishukuru sana TRC kwa kutekeleza agizo la serikali ya kuwajali wanyonge na kuinua maisha ya wananchi wa hali ya chini ili kwa pamoja kuweza kuzidi kukuza uchumi wananchi.