Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHIRIKA LA RELI TANZANIA LAKAMILISHA MAADHIMISHO YA WIKI YA TRC


news title here
23
December
2019

Shirika la Reli Tanzania – TRC lakamilisha Wiki ya TRC ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa kutoa elimu na ufafanuzi kuhusu huduma zitolewazo na miradi inayosimamiwa na Shirika kuanzia tarehe 12 - 20 Desemba 2019.

Mwaka huu Wiki ya TRC imeadhimishwa kwa kufanya ziara katika vyombo vya habari vikiwemo Radio na Televisheni tofauti ambazo ni TBC1, Clouds TV, Channel Ten, Azam TV, ITV, Radio One, TBC Taifa na Magic FM, aidha shirika lilikuwa likitoa elimu kupitia maadhimisho hayo katika Mitandao ya Kijamii na Tovuti ya Shirika.

Wiki ya TRC ilifunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kwa kufanya mkutano na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Habari Maelezo uliopo jengo la kumbi za mikutano la JNICC jijini Dar es Salaam Desemba 12, 2019.

Mkurugenzi Mkuu alieleza mafanikio ya Serikali kwa kipindi cha miaka mine katika sekta ya reli ambapo waandishi pia walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR Dar es Salaam – Makutupora, Mradi wa uboreshaji wa reli ya kati – TIRP, kurejea kwa huduma ya usafiri Dar es Salaam – Moshi na Dar es Salaam – Kampala, pamoja mikakati ya Serikali ya kujenga reli ya Kisasa kutoka Mwanza – Isaka, Mtwara – Bambabay na reli za mijini katika jiji la Dar es Salaam na makao makuu ya nchi Dodoma.

“Hata hivyo bado kuna mafanikio katika reli ya kati ambapo jumla ya tani 1,456,537 katika reli ya kati zimesafirishwa na kwa upande wa treni za abiria mikoani jumla ya abiria 578,439 wameongezeka kwa mwaka 2018/19” Hayo yamebainishwa na Mkrugenzi Mkuu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Habari Maelezo.

Mbali na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara TRC Bwana Henry Machoke, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC Bi. Jamila Mbarouk, Meneja Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR Dar es Salaam – Morogoro Mhandisi Machibya Masanja, Meneja Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati – TIRP Mhandisi Mlemba Singo ni miongoni mwa watoa mada walioshiriki katika ziara ya vyombo vya habari kuelezea huduma na miradi ya Shirika katika wiki ya TRC.

Halikadhalika kupitia wiki hiyo Meneja Mradi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro Mhandisi Machibya Masanja alifafanua kuwa Shirika limekamilisha usanifu kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kutoka Tanga - Arusha - Musoma, Mtwara – Bamba Bay pamoja na reli za mjini katika jiji la Dar es Salaam, pia Shirika linaendelea na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tabora – Isaka, Tabora – Kigoma, Kaliua – Mpanda – Kalema, Uvinza – Msongati Burundi na Isaka – Kigali Rwanda alipokuwa katika kipindi cha ‘Morning Magic’ cha Magic FM.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kwa niaba ya Shirikaametoa shukurani kwa vyombo vya habari nchini pamoja na waandishi wa habari kwa ushirikiano wanaotoa kutangaza na kuhabarisha umma kuhusu jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za usafiri wa reli nchini kupitia miradi mikubwa ya kimkakati yenye lengo la kuleta mapinduzi katika uchumi wa nchi ifikapo 2025. Mkurugenzi Mkuu anatoa rai kwa watanzania wote kwa pamoja kuwa walinzi wa miundombinu ya reli kwani ni mali yao na ni jukumu la watanzania kutunza miundombinu hiyo kwa manufaa yavizazi vijavyo.