Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SHIRIKA LA RELI TANZANIA LAENDELEA NA MAFUNZO KUHUSU NAMNA YA KUZUIA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA CORONA


news title here
19
March
2020

Shirika la Reli Tanzania - TRC laendelea na mafunzo kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona kwa kutoa elimu ya mambo ya kuzingatia ili kujikinga na maambukizi katika Stesheni ya Kamata iliyopo Kariakoo Gerezani jijini Dar es Salaam Machi 19, 2020.

Lengo la mafunzo ni kuhakikisha abiria wanaotumia usafiri wa treni za mjini na mikoani wanapata uelewa wa kutosha kuhusu namna bora ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona vilivyoingia nchini hivi karibuni pamoja na kutekeleza maagizo ya serikali kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Mafunzo hayo yanatolewa na wataalam wa afya kutoka Zahanati ya Reli makao makuu wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Zahanati Daktari Peter Mathew ambapo awali mafunzo hayo yaliendeshwa kwa wafanyakazi pamoja na uongozi wa Shirika katika ofisi za makao makuu jijini Dar es Salaam.

Shirika linaendelea na jitihada hizo katika maeneo yote nchini ambayo yamepitiwa na reli hasa katika stesheni za reli ambazo zimekuwa na idadi kubwa ya abiria wanaotumia usafiri wa treni katika reli ya kati kuanzia Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Kigoma, Mpanda na Mwanza pamoja na reli ya Kaskazini kuanzia Ruvu, Tanga, Moshi hadi Arusha, halikadhalika Shirika linaendelea na utoaji elimu kwa wafanyakazi kupitia hospitali za Shirika zilizopo maeneo hayo.

“Shirika lilianza kutoa elimu ya afya kwa wafanyakazi wake pamoja na wananchi wanaoishi pembezoni mwa reli, tunatoa vipeperushi na matangazo ili kuhakikisha ugonjwa hauingii kupitia sisi, ndani ya treni zetu kuna vyumba vya huduma pamoja na mtaalamu wa afya” alisema Dkt. Peter

Dkt Peter aliongeza kuwa “anapotokea mgonjwa wa Corona tutampatia huduma zote kwenye chumba cha huduma kwa kumtenga na tutamshusha katika vituo vyetu vya afya vilivyopo njiani, Morogoro, Dodoma, Itigi, Tabora, Kigoma, Mwanza, Tanga pamoja na Moshi”

Aidha, miongoni mwa hatua ambazo Shirika limechukua mpaka sasa ni pamoja na kuhakikisha abiria wanaosafiri kwa treni zote za mjini na za mikoani wanakaa kulingana na idadi ya viti (Level Seat) ili kuondoa msongamano wa abiria unaoweza kuongeza kasi ya maambukizi, sambamba na hilo shirika limeweka maji na dawa ya kuosha mikono kwa ajili ya kuua virusi vya Corona katika maeneo ya kazi na Stesheni zote nchini.

“tumeanza utekelezaji wa maagizo ya serikali kwa kuhakikisha abiria wanakaa kulingana na idadi ya viti (level seat) ili kuleta usalama wa abiria wetu na kupunguza uwezekano wa abiria kupata maambukizi ya virusi vya Corona, pia kila abiria anayeingia ndani ya treni zetu lazima anawe mikono kwa maji safi na sabuni” alisema Meneja wa treni za mjini na mikoani Iddy Mzugu

Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC BI. Jamila Mbarouk ameeleza kuwa kinachofanyika ni kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona ukizingatia kuwa Shirika linatoa huduma ya usafiri wa abiria, hivyo Shirika linaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, vipeperushi na mikutano ya ana kwa ana na abiria, wananchi na wafanyakazi katika maeneo ya Stesheni, kambi za ujenzi na maeneo ya pembezoni mwa reli