Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHIRIKA LA RELI LASITISHA HUDUMA YA USAFIRI WA TRENI KWA RELI YA KATI


news title here
05
February
2020

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ametangaza kusitisha huduma za usafiri wa treni za abiria na mizigo kwa reli ya kati kutokana na uharibifu wa njia ya reli uliosababishwa na mafuriko maeneo ya Kilosa, Igandu, Dodoma na Makutupora, taarifa hiyo imetolewa wakati wa mkutano na wandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano makao makuu TRC jijini Dar es salaam Januari 5, 2020.

Mvua hizo zinazoendelea kunyesha ukanda wa kati kuanzia tarehe 27/01/2020 katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha kufurika kwa mto Mkondoa na kuleta uharibifu mkubwa katika njia ya reli hasa maeneo ya Kilosa (Morogoro), Gulwe (Mpwapwa), Igandu, Zuzu na Makutupora (Singida). Takribani maeneo 26 yameathirika kati ya hayo 10 yako katika hali mbaya ambapo tuta la reli na baadhi ya Makalavati yamezolewa na maji.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amewaeleza waandishi wa Habari kuwa tayari jitihada za awali zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kujaza vifusi katika maeneo yaliyoathirika eneo la Kilosa – Igandu ili kurudisha mawasiliano katika maeneo hayo, sambamba na hili Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa mkakati wa kudumu uliopo ni kuhamishia reli milimani ili kuhakikisha reli inakuwa salama muda wote.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TRC hivi karibuni alilazimika kutembelea katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo na kujionea hali halisi ambapo wahandisi kutoka shirika la reli nchini, wahandisi wa mkandarasi kampuni za CCECC inayokarabati reli ya kati, pamoja Mkandarasi wa Reli ya Kisasa – SGR Kampuni ya YAPI Merkezi ambao wote kwa pamoja wanashirikiana kuweza kurejesha huduma ya usafiri katika maeneo hayo.

Kutokana na hali hiyo Shirika limefanya jitihada za kuwasafirisha kwa mabasi kuelekea Dar ees Salaam abiria wote waliokwama Dodoma, halikadhalika abiria waliokata tiketi kwa ajili ya safari wamerudishiwa fedha zao ili waweze kutafuta usafiri mwingine wa kuwafikisha waendako.

Shirika linaomba radhi kwa wadau wa sekta ya miundombinu ya reli kutokana na kusimama kwa huduma za uchukuzi wa abiria na mizigo hasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma mpaka hapo hali itakapotengemaa, Shirika litawajulisha wadau wa sekta ya miundombinu ya reli, ikizingatiwa kuwa bado mvua zinaendelea kunyesha.