Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SHIRIKA LA RELI LAENDELEA NA KAMPENI ZA UELEWA KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA ALAMA ZA USALAMA WA RELI


news title here
28
January
2020


Shirika la Reli Tanzania TRC limezindua kampeni ya uelewa kuhusu usalama wa miundombinu ya reli, matumizi sahihi ya alama za njia ya reli na mfumo mpya wa kukusanya maoni, katika ukumbi wa mikutano ofisi ya makao makuu jijini Dar es Salaam Januari 28, 2020.

Lengo la Kampeni hii ni kutoa uelewa kwa watumiaji wa miundombinu ya reli wakiwemo madereva, watembea kwa miguu na wananchi kwa ujumla katika maeneo ambayo miundombinu ya reli imepita ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya alama za usalama wa njia ya reli pamoja na kuboresha huduma zitolewazo na Shirika.

Kampeni hiyo imezinduliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Focus Makoye Sahani ikiwa ni muendelezo wa kampeni zinazofanywa na Shirika kila mwaka kutoa elimu yenye lengo la kupunguza na kuzuia ajali, uharibifu na hujuma katika miundombinu ya reli, ambapo wataalamu kutoka Ofisi ya Usalama wa Reli, Mambo ya Kijamii, Jeshi la Polisi Reli na Ofisi ya Habari na Uhusiano TRC hushiriki katika kampeni hizo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa changamoto zimekuwa nyingi katika shughuli za reli tangu huduma ilipoanza katika reli ya Dar es Salaam - Moshi lakini vyombo vya ulinzi na usalama kupitia kikosi cha polisi reli vimekuwa vikifanya doria mara kwa mara katika njia ya reli kabla ya treni kupita, Shirika linaiomba serikali kuanzia mwananchi mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa kuendelea kutoa ushirikiano na kuwa walinzi wa miundombinu ya reli katika maeneo yanayopita reli kote nchini.

Kamanda kikosi cha Reli Kamishna Msaidizi Stanley Kuliamo ametoa wito kwa wafugaji, wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya reli, pamoja na watembea kwa miguu na madereva kuwa makini wanapo katika makutano ya reli na barabara.

“Natoa rai kwa wananchi tushirikiane kwa pamoja kuwa walinzi wa miundombinu ya reli pia naomba wazingatie yafuatayo; waache kuhujumu miundombinu ya reli, madereva wapunguze mwendo katika makutano ya reli ama vivuko na kuzingatia alama za barabarani, wananchi waache tabia ya kukaa karibu na reli na kwa wafanyabiashara ni hatari kwa usalama wao kufanya biashara katika maeneo ya reli” alisema Kamanda Kuliamo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha usalama na Ulinzi wa Reli Mhandisi Maizo Michael Mgedzi amefafanua aina za ajali zinazoweza kutokea kama uelewa wa usalama wa reli usipozingatiwa; treni inaweza kupinduka kama wananchi wakiweka mawe, na vitu vizito katika njia ya reli, kuiba vifaa vya reli, kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya reli, uzembe wa madereva

Mhandisi Maizo Mgedzi amewaasa wananchi kuonesha ushirikiano kwa kutoa taarifa katika vituo vya Polisi na kupiga simu ya bure 0800110042 kuripoti vitendo vya kihalifu katika mundombinu ya reli, pia amewaomba wanahabari kuendelea kuelimisha umma kuhusu jukumu la ulinzi wa miundombinu ya reli lakini pia kuzingatia alama za usalama wa reli.

Mkuu wa kitengo cha Sheria TRC Bi. Veronica Sudayi amesisitiza kuwa Shirika halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote anayehujumu miundombinu ya reli, ambapo adhabu yake ni faini isiyopungua Shilingi Milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka 3 jela au vyote kwa pamoja.

“kutokujua sheria sio kinga ya kutopata adhabu lakini tunawapenda wananchi ndio maana tunawakumbusha kwa kufanya kampeni hii endelevu kila mwaka ili kila asiyejua apate kujua na kutunza miundombinu ya reli na kuwa balozi wa wengine” alisema Veronica.

Naye mtaalamu wa Masuala ya Kijamii Bwana Lazaro Leodgard Otaru ameeleza jinsi ofisi ya Jamii TRC inavyofanya kazi kwa kutoa elimu kuhusu namna ya kuwasilisha maoni na malalamiko yanayotokana na shughuli za kila siku za shirika, kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mtambuka ikiwemo afya, jinsia na kutoa ufafanuzi au utatuzi wa changamoto zinazoripotiwa na wananchi baada ya siku 15.

Kampeni hii ya uelewa itahusisha mikutano ya ana kwa ana na wadau wa sekta ya reli ambao ni madereva, watembea kwa miguu na wananchi kwa ujumla pamoja na vyombo vya habari vikiwemo redio, televisheni,magazeti na mitandao ya kijamii nchi nzima kuanzia Januari 29, 2020.