Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SHANGWE: WANAKIJIJI PANGAWE NA MIKESE MKOANI MOROGORO, WALIPWA FIDIA KUPISHA UJENZI WA RELI YA KISASA


news title here
21
August
2020

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la ulipaji wa fidia kwa awamu katika maeneo ya Morogoro vijijini ili kupisha ujenzi wa Reli ya kisasa - SGR kipande cha Dar es Salaam - Morogoro, Agosti hivi karibuni 2020.

Zoezi hilo la ulipaji wa fidia limeleta shangwe na kuwafurahisha wakazi wa kijiji cha Pangawe na Mikese kwa kuwa wamekua wakisubiri kwa hamu kupatiwa hundi zao.

Wananchi hao wameonyesha ushirikiano mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi katika maeneo husika na kuhakikisha wamekamilisha nyaraka zilizohitajika na maafisa kutoka TRC ili kuendesha zoezi kwa uhakiki na usahihi kuepusha migogoro ya aina yeyote kujitokeza.

Aidha zoezi hilo lilisimamiwa pia na wenyeviti wa kijiji, watendaji, wathamini kutoka wizara ya ardhi pamoja na maafisa wa Polisi reli ili kuweza kuhakikisha hali ya usalama wa raia katika zoezi.

Mtendaji wa Kijiji cha Mikese Bw. Haji Maridadi amesema kuwa mkoa wa Morogoro ni mkoa wa Kilimo hivyo upishaji huo wa ujenzi wa reli ya kisasa utanufaisha wengi endapo usafiri wa reli ya mwendokasi (SGR ) ikianza kutumika kwa kupata urahisi wa usafiri wa haraka kwa wananchi mkoani hapo.

“Wanakijiji wamefurahi sana kwa kupatiwa malipo yao , serikali hii ni ya maendeleo zaidi “ alisema Bw. Maridadi .

Naye Afisa wa Masuala ya Jamii kutoka TRC Bi. Lightness Mnguru ameeleza kuwa malipo hayo yanafuata taratibu na haki za wanajamii na hali hiyo huepusha malalamiko ya wananchi waliopitiwa na mradi huo wa SGR

Wananchi wametoa pongezi kwa Serikali pamoja na kuushukuru uongozi na wafanyakazi wa TRC kwa jitihada na kazi nzuri wanazozifanya katika kusimamia miundombinu ya reli na kuhakikisha kila mwananchi analipwa stahiki zake.