Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SGR YAZIDI KUWA CHACHU YA MAENDELEO WILAYANI KILOSA


news title here
15
October
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendela kuwapatia malipo ya fidia wananchi wa wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ili kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora kwenye zoezi la malipo ya fidia lililofanyika wilaya ya Kilosa hivi karibuni Oktoba, 2022.

Zoezi hilo la malipo ya fidia limefanyika baada ya wananchi kutwaliwa maeneo yao kwaajili ya maeneo ya kuchimba vifusi katika mradi wa SGR ambapo wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo kijiji cha Milima boma, Munisagara pamoja na kijiji cha Kidete walipatiwa stahiki zao.

Afisa Ardhi kutoka TRC Bi. Benlulu Lymo amesema kuwa maeneo yaliyotwaliwa ni pamoja na ardhi, mashamba, mazao pamoja na nyumba ambapo wananchi wanakabidhisha nyaraka husika kabla ya kukabidhiwa malipo yao.

“Kwa aliye na nyumba na kiwanja tunahakikisha nyaraka zote za umiliki ni sahihi ndipo anapatiwa malipo yake” alisema Bi. Benlulu.

Aidha, Bi.Benlulu alisema kuwa mwananchi kukabidhisha nyaraka hizo ni kufuata taratibu ili kuepusha udanganyifu wowote utakaojitokeza ama kuleta migogoro kwa familia.

Naye Afisa masuala ya jamii Bi. Eveline Kamugisha ameeleza kuwa wananchi wanaendelea kupewa elimu ya kutunza maeneo yao kwa kufanya maendeleo vijijini pamoja na miundombinu ya reli.

“Tunaendelea kuwasihi wananchi kutunza miundombinu ya reli na kutolima pembezoni mwa njia ya reli ili kuepusha mmomonyoko wa udongo kipindi kijacho na kuharibu njia ya reli” alisema Bi. Eveline.

Vilevile mwananchi kutoka katika kijiji cha Munisagara ambae pia ni mfanyakazi wa kibendera kutoka katika kampuni ya mkandarasi wa SGR ya Yapi Merkezi Bw. Angero Sekeni amesema kuwa mradi huo wa SGR umeleta maendeleo vijijini kwa kutoa ajira na pia biashara kuongezeka.

“Wilaya ya kilosa inazidi kuendelea kutokana na mradi huu na wageni kuja kwa wingi kuwekeza kwenye biashara za nyumba za kulala wageni, nyumba za kupangisha, vituo vya mafuta na maduka” alisema Bw. Angero.

Wananchi wanazidi kupata mbinu za kufanya maendeleo vijijini kupitia mradi huo wa ujenzi wa SGR pia usafirishaji kuwa na urahisi pindi treni ya kisasa itakapoanza kutumika.