Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SGR YAONESHA MCHANGO WA UHANDISI KATIKA MAENDELEO YA AFRIKA


news title here
15
September
2026

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema limetekeleza kwa asilimia 60 ajenda ya kuunganisha miji ya Afrika ifikapo mwaka 2063 ikiwa ni sehemu kuu ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika (AU), inayolenga kuleta maendeleo, amani, na utangamano wa kiuchumi barani.

Mkurugenzi Mkuuwa TRC, Mha. Machibya Shiwa, amuelezea hayo Makamu wa Rais wa pili wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, alipotembelea banda la maonesho la TRC wakati wa maadhimisho ya 12 ya wiki ya Wahandisi UNESCO -Afrika na Kikao cha 10 cha Wahandisi Afrika kinachofanyika Septemba 14-17, 2026 Jijiji Dar es Salaam.

Mha.Machibya, ameeleza kuwa mradi wa SGR inadhihirisha jinsi uhandisi, sayansi na teknolojia vinavyoweza kutatua changamoto za usafiri na kuboresha maisha ya wananchi Kwa

Kuunganisha watu na fursa mbalimbali.

"Tanzania imetekeleza Azimio la Afrika kwa zaidi ya asilimia 60 linalotaka Miji yote mikuu ya Afrika ifikapo 2063 iwe imeungana kwa kutumia reli ya SGR, kuunganisha miji mikuu ya Afrika kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kufungua fursa za kibiashara, utalii, kilimo, viwanda na uwekezaji" amesema Mha. Machibya.

Mha.Machibya ameongeza kuwa usafiri wa reli umeipa nafasi Tanzania ya kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki na Kati kwa kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani

"Kwa kusafirisha abiria wengi kupitia SGR na mizigo ambayo ilikuwa ikisafiri kupitia barabara imeweza kusaidia kupunguza msongamano wa magari, uharibifu wa barabara, matumizi ya mafuta, gharama za usafirishaji na uchafuzi wa Mazingira "amesema Mkurugenzi Mkuu wa TRC.

Ameongeza kusema kuwa ujenzi wa miundombinu imara unategemea maarifa, ubunifu na utaalamu wa wahandisi na pia vijana, wanawake na wataalamu wa ndani kupata ujuzi na kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo.

Ameongeza kuwa, katika kuendana na Kaulimbiu ya Wiki ya Uhandisi inayosisitiza umuhimu wa kutumia ubunifu, ushirikishwaji na uendelevu katika kujenga maendeleo ya Afrika , TRC imedhihirisha hilo kuwa ujenzi wa SGR ni zaidi ya reli, ni mradi unaolenga kuunganisha watu na fursa, kuchochea uchumi na kujenga mfumo wa usafiri wa kisasa na endelevu.