TRC YACHUKUA TAHADHARI KULINDA MIUNDOMBINU YA RELI
September
2026
Kitengo cha mazingira cha Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kushirikiana na mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dr. Elly Ligate, Septemba 10, 2026 wameendelea na zoezi la uhamasishaji kuhusu usimamizi endelevu wa ardhi na uhifadhi kwa jamii katika vyanzo vya maji kando ya miundombinu ya reli na upandaji wa nyasi jamii ya Juncao katika mto Lumuma wilaya ya Kilosa kwa lengo la kudhibiti mmomonyoko wa ardhi.
Lengo kuu la zoezi hili ni kuimarisha uelewa na ushiriki wa jamii katika usimamizi endelevu kupitia urejeshaji wa ardhi, uhifadhi wa udongo na maji, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabia nchi na usimamizi bora wa mifugo.
Hatua hizi zinalenga kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuboresha maisha ya jamii na kulinda miundombinu ya reli.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Salome Mkinga amesema zoezi hili la utunzaji wa mazingira ya Kilosa litasaidia kuepuka athari ambazo zitaletwa na mafuriko kama ambavyo zimetangazwa na mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
"Huu mkakati utasaidia sana kuboresha miundombinu na itasaidia kupunguza athari ambazo zinatarajiwa kutokea kwenye mvua kubwa ya el nino" ameongeza Mhe. Mkinga.
Mhe. Salome amewasisitiza wananchi wa Kilosa kushirikiana kwa pamoja na viongozi katika utunzaji wa mazingira ili kuweka ustawi mzuri wa maisha ya sasa na kizazi kijacho.
Mratibu wa Jamii na Mazingira TRC Mhandisi Dr. Veronica Mirambo amesema upandaji wa nyasi jamii ya Juncao utasaidia kurejesha ekolojia ya mto Lumuma ambao umekua ukishambuliwa na mafuriko na kusababisha hali hatarishi ya miundombinu ya reli (MGR na SGR) katika daraja la Kidete.
"Kwahiyo kupitia upandaji huu wa majani ya Juncao katika kingo za mto Lumuma utaenda kutengeneza na kuimarisha kingo za mto kwani majani haya yana mizizi mirefu yatasaidia sana kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika miundombinu ya reli" ameongeza Dr. Veronica.
Zoezi la uelimishaji jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na miundombinu iliyo kando kando ya reli ni endelevu ambapo mpaka sasa limewafikia wananchi wa vijiji vya Mkadage, Munisagara, Mzaganza,Msisi na Kidete wilaya ya Kilosa na litaendelea katika Wilaya ya Mpwawa.

