TRC YALETA HAMASA YA MAENDELEO KWA WANANCHI TABORA
October
2023
Shirika la Reli Tanzania linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zimetwaliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa - SGR kipande cha nne Tabora - Isaka, Oktoba 2023.
Katika zoezi la ulipaji fidia takribani shilingi milioni Mia tatu na nane zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi 251 wa vijiji vya Kakola, Magoheko na Ikomwa wilaya ya Tabora Mjini na vijiji vya Kayombo na Malolo za wilaya ya Nzega mkoa wa Tabora.
Kutokana na zoezi la ulipaji fidia wananchi wa Tabora wamefurahia kwa kua malipo hayo yamefanyika wakati muafaka, kwa kua hivi karibuni msimu wa kilimo unaanza, wananchi watanunua mbegu, kulipa vibarua na kuendeleza shuguli za ufugaji na wengine kujenga nyumba za kisasa kwa kuwa wanakipato cha kuwezesha cha kutosha na kuendeleza shuguli nyingine za kijamii.
Pamoja na hayo afisa ardhi kutoka Shirika la Reli Tanzania Msanifu Solomon Obed amesema kuwa maeneo yaliotwaliwa na wananchi kulipwa wakati muafaka ni kwa ajili ya kupisha ujenzi wa njia kuu ya Reli ya SGR .
"Zoezi la ulipaji fidia linaendelea vizuri na wananchi wamekua waelewa katika kushirikiana na wataalamu kuanzia awamu ya Kwanza ya uthamini wa Mali na ardhi mpaka awamu hii ya malipo ya fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zimetwaliwa kupisha ujenzi huu wa njia kuu ya Reli" Amesema Msanifu Solomon.
Naye Afisa mazingira kutoka Shirika la Reli Tanzania Bi. Raya Issa ameeleza kuwa kutokana na kampeni endelevu za uhamasishaji zinazofanywa na TRC kushirikiana na wadau mbalimbali kwenye Jamii zimehamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa SGR katika maeneo mbalimbali yanayopitiwa na mradi .
"Zoezi la ulipaji fidia limekuwa jepesi sana kwasababu wananchi wamekua wakielimishwa na kuhamasishwa kuhusiana na maswala ya kijamii na utunzaji mazingira katika ujenzi wa SGR" Amesema Bi. Raya.
Bwana Rafael Bundala mwenyekiti wa kijiji cha Kayombo ameongeza kuwa malipo ya fidia yamekuwa mkombozi wa uchumi na maendeleo ya wanakijiji cha Kayombo haswa katika shughuli za kilimo na ufugaji.
"Ujio wa SGR kwa wananchi umeleta matumaini na hamasa katika maendeleo. Zoezi la ulipaji fidia ni endelevu katika ujenzi wa SGR ili kuhakikisha wananchi wanapata stahiki na haki pindi ardhi zao zinatwaliwa.