Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​SGR KUWA KITOVU CHA UKUAJI WA BIASHARA TANZANIA


news title here
06
July
2023

Mkurugenzi wa Miundombinu na Ujenzi Shirika la Reli Tanzania - TRC Mhandisi Machibya Masanja pamoja na Mkurugenzi wa Ishara, Mawasiliano na Umeme TRC Mhandisi Mateshi Titto watembelea banda la TRC lililopo katika viwanja vya Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa - Sabasaba jijini Dar es Salaam Julai, 2023.

Mhandisi Machibya alisema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR unaendelea katika vipande vyote vya awamu ya kwanza vyenye urefu wa kilomita 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

“ujenzi kwa kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro umefikia 98.9%, kipande cha pili Morogoro - Makutopora umefikia 94.19%, kipande cha tatu Makutopora - Tabora ujenzi umefikia 7.88%, kipande cha nne Tabora - Isaka ujenzi umefikia 3.03% na kipande cha tano Isaka - Mwanza ujenzi kimefikia 33.3%.

Aidha, Mhandisi Machibya alisema ujenzi wa SGR awamu ya pili mkandarasi yupo eneo la ujenzi kwa kipande cha kwanza kinachoanzia Tabora - Kigoma kwaajili ya ujenzi wa kambi na kupeleka vifaa vya ujenzi tayari kwa kuanza kazi.

Pia Mhandisi Machibya aliongeza kuwa Shirika limeshaanza mchakato wa manunuzi kwaajili ya kipande cha pili kutoka Uvinza hadi Gitega nchini Burundi.

"Ujenzi wa SGR utakuza biashara ya Tanzania na nchi jirani za Demokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi kwakuwa ni wateja wetu wa kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam na itajengwa bandari kavu Isaka, Uvinza na Katosho ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa nchi jirani "alisema Mhandisi Machibya .

Naye Mkurugenzi wa Ishara, Mawasiliano na Umeme Mhandisi Titto ameeleza kuwa usafirishaji wa mizigo na abiria kwa kutumia reli ya kisasa SGR utakuwa salama, na kwa upande wa ubebaji wa mizigo kutakuwa na mizani iliyowekwa taarifa za uwezo wa mabehewa kubeba mzigo pamoja na mfumo wa mizani ambao utatoa taarifa ya uzito wa mzigo na kudhibiti kupakia mzigo zaidi ya uwezo wa behewa kwa kutoa viashiria vya sauti, vilevile kwa upande wa abiria kutakuwa na mfumo utakaowezesha kufuatilia matukio yote ndani ya stesheni, kujua muda wa treni kuondoka na mahala ilipo.

"Kutakuwa na mifumo ya CCTV kamera itakoyorekodi matukio yote kwa kila stesheni hivyo kumuhakikishia usalama abiria na mizigo, abiria watarahisishiwa ukataji wa tiketi, wataweza kutumia mashine mfano wa ATM, wataweza kukata tiketi mtandaoni na kukata tiketi dirishani" alisema Mhandisi Mateshi."

Mifumo ya uendeshaji wa treni ya kisasa utakuwa na tija kwa Shirika na wafanyabiashara kwa kuwawezesha kufuatilia mizigo yao inapopakiwa, kujua upo wapi na utafika kituo cha mwisho saa ngapi ili mfanyabiashara aweze kupanga mipango yake." aliongezea Mhandisi Matesh.

Maonesho ya 47 ya Biadhara ya Kimataifa yatafunguliwa rasmi tarehe 5 Julai 2023 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 13 Julai 2023.