Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

SGR KULINUFAISHA JIJI LA DODOMA


news title here
20
May
2024

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na majaribio pamoja na shughuli mbalimbali za maandalizi ya kuanza uendeshaji wa treni za SGR ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai, 2024.

Katika maandalizi ya kuanza shughuli za uendeshaji moja ya mkakati ni kuendelea kwa kampeni ya uelemishaji na uhamasishaji wa kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kufuatia zoezi la uwekaji na ufungaji mageti wa njia ya treni ya SGR kipande cha pili cha Morogoro - Makutupora.

Lengo la kampeni ya uhamasishaji ni kujenga uelewa ,ushirikiano na kupokea mapendekezo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano baina ya TRC na viongozi mbalimbali katika kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Reli pamoja na Usalama wa wananchi na Mali zao.

Aidha ,kufuatia kampeni ya uelewa viongozi mbalimbali wameweza kuonesha ushirikiano katika kuhakikisha treni ya SGR inachagiza maendeleo mbalimbali katika jamii na nchi kwa ujumla .

Akiongea na maafisa wa TRC wakati wa kampeni ya uelewa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jiji Mhe. Jabir Shekimweri amesema ujenzi wa SGR unatarajiwa kuwa chachu kubwa katika kuongeza thamani ya Jiji la Dodoma kutokana na ukuaji wa sekta mbalimbali.

Shekimweri amesema kutokana na Jiji la Dodoma kijografia kuwa katika ya nchi treni ya SGR itasaidia mzunguko wa watu kuwa mkubwa kutokana na ufanisi na urahisi wa miundombinu ya SGR.

"Kitaifa Dodoma ni katikati ya nchi , SGR inaenda kupunguza umbali wa safari kutoka sehemu moja kwenda nyingine, Serikali imehamia Dodoma kwa hiyo ujio wa SGR utaongeza ufanisi wa serikali kwa kupunguza masaa ya kusafiri kwa watumishi na wananchi wanaofuata huduma za Serikali" Alisema Shekimweri.

Shekimweri ameongeza kuwa ujio wa SGR utaongeza ukuaji wa sekta ya kilimo haswa kilimo cha zao la zabibu ambalo linazalisha mvinyo na pia zao la alizeti linalo zalisha Mafuta ya kupikia na bidhaa nyinginezo.

"SGR itasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao , Dodoma tuna fursa ya kilimo cha zabibu ambayo inazalisha mvinyo,pia Dodoma inakiwanda cha mbolea cha "intra - Com Fertilizers " ambacho kwa mwaka kinazalisha tani takribani 1.2 kwa mwaka ,kwa hiyo SGR itaongeza uzalishaji wa bidhaa hizi nakuweza kufika nchi zingine za Afrika" Alisema Mhe. jabir.

Mhe. Shekimweri amehitimisha kwa kusema kuwa usafiri wa treni ya SGR utapunguza ugumu wa maisha ya wananchi kutokana na kupungua kwa bei za usafishaji ambapo kwa Sasa bei za bidhaa nyingi katika jiji la Dodoma ni kubwa kutokana na bei za usafirishaji.

Kampeni ya Uelewa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama inaendelea katika kipande cha pili cha ujenzi wa SGR ( Morogoro - Makutupora ) ikilenga kufanyika katika Wilaya Saba ambazo ni Mvomero, Kilosa, Mpwapwa, Chamwinwo, Dodoma Jiji, Bahi na Manyoni.