RIPOTI ZAFANANA NA UHALISIA; MRADI WA SGR MOROGORO – MAKUTUPORA WAFIKA 70%
August
2021
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya Uchukuzi Bw. Gabriel Migire ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Morogoro – Makutupora katika eneo linalojengwa Mahandaki Kilosa mkoani Morogoro Agosti 29, 2021.
Katibu mkuu ameeleza kuwa lengo la ziara yake ni kukagua maendeleo ya mradi pamoja na kujiridhisha na ripoti anazopokea kama zinafanana na uhalisia ambapo amesema kuwa hakuna tofauti ya ripoti anazopokea na uhalisia wa utekelezaji wa mradi huo.
“Lengo la ziara yangu ni kujionea kinachoendelea kwa kuwa huwa ninapokea taarifa mara kwa mara ya mradi huu, nimekuja ili nione yale ambayo yanaelezwa kwenye makaratasi yanafanana na hali halisi kwenye utekelezaji” alisema Katibu Mkuu, Gabriel Migire
Migire aliongeza kuwa “Nimekuta hakuna tofauti na pengine yanayoripotiwa kwenye karatasi ni machache kuliko yale yanayofanyika”
Katibu mkuu amewataka watanzania kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi mara baada ya mradi huo kukamilika kwa kuandaa mazingira mazuri na kujipanga kwa ajili ya kuwekeza na kufanya biashara katika maeneo ambayo mradi huo unapita
“Miundombinu hii serikali inaiweka ili kuwezesha ubebaji wa mizigo na kuchagiza biashara, lakini wanaofanya biashara sio serikali ni wananchi na sekta binfasi, tunavyozungumzia asilimia 90 Dar es Salaam – Morogoro na asilimia 70 Morogoro - Makutupora maana yake na wao maandalizi yao yanatakiwa yawe yamefika pazuri kwenye kuandaa biashara zao, sekta binafsi zinatakiwa zione fursa na namna ya kuzitumia”
Aidha, Katibu mkuu ameeleza mipango na mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo katika mradi huo mara baada ya kukamilika kwake.
“Tunafanya kazi na wizara nyingine, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kituo cha uwekezaji kimeanza kuratibu uwekezaji kwenye ‘Corridor’ nzima ya reli na kushawishi wadau wote wanaoweza kufanya uwekezaji na kutumia hizo fursa” alisema Bw. Migire
Katibu mkuu amewaomba wananchi kuwa sehemu ya mradi huo kwa kulinda miundombinu ya reli kwani mradi huo si wa serikali bali ni wa wananchi na unatumia fedha zao kutekelezwa
“Hizi ni fedha za wananchi, wanapaswa kulijua hilo na kulinda mali yao, kinachojengwa ni cha kwao wanapaswa kukilinda kama wanavyolinda mali zao” alisema Bw. Migire
Naye Meneja Mradi wa SGR kipande hiko Mhandisi Mateshi Tito amesema kuwa mradi unaendelea vizuri ambapo pamoja na kazi nyingine kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni ujenzi wa msongo mkubwa wa Kilovoti 220 kwa ajili ya kuleta umeme kwenye mradi, ujenzi ambao unaanzia ya Msamvu hadi Kintinku na umegawanjika sehemu mbili, sehemu ya kwanza Morogoro - Dodoma ambayo ujenzi wake umefikia 53% na sehemu ya pili Dodoma - Makutupora ambayo imefikia 52%.