RC CHALAMILA APONGEZA HUDUMA YA TRENI ZA JIJINI DAR ES SALAAM
November
2023
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametembelea Shirika la Reli Tanzania – TRC kuona huduma ya usafiri wa treni ya mjini inayofanya safari kutoka Kamata kuelekea Pugu jijini Dar es Salaam Novemba 8, 2023.
Mkuu wa mkoa amefanya ziara kwa lengo la kuona huduma zinazotolewa na TRC, kusikiliza changamoto zilizopo
katika usafiri ili kupata utatuzi hususani wakati wa kipindi cha mvua za masika ambapo ameipongeza TRC kwa kutoa huduma ya usafiri ambao umekuwa mkombozi kipindi cha mvua nyingi.
“Lengo ni kwamba nataka nikajionee changamoto wanazopata wananchi ndani ya treni, usafiri huu ni mzuri sana lakini nataka nikasikie kwa wananchi wenyewe changamoto gani wanapata lakini pia wanipe ushauri ili tuweze kuboresha kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Chalamila
Mkuu wa mkoa alipata fursa ya kusafiri na treni ya Pugu kuanzia Stesheni ya Kamata hadi Pugu na kutoka Pugu
nadi Kamata na kuzungumza na abiria waliosafiri katika treni. Chalamila ameipongeza TRC kwa huduma inazotoa
na kuishukuru kwa kuwawezesha walimu kupanda treni bure na kuwataka waendelee kufanya hivyo.
“Niwapongeze kwa kazi hii kwasababu nafahamu historia ya reli hii, haya mabehewa yalikuwa ya daraja la pili na yalikuwa na vitanda, ninyi ili kuwapa huduma wananchi mkaamua kuyatengeneza ili yakidhi mahitaji” alisema Bwana Chalamila
Chalamila ameeleza baadhi ya sababu zinazopelekea changamoto ya usafiri ikiwemo barabara kutoka mjini kati hadi Gongo la Mboto inayojengwa na kupelekea njia kuwa finyu kwasababu mkandarasi hajajenga njia mbadala
ya kutosha kupitisha magari. Hali hiyo imepelekea kuwepo na wingi wa abiria wanaosafiri na treni na kusababisha msongamano mkubwa katika mabehewa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli ameeleza kuwa TRC inatoa huduma ya usafiri wa abiria kwa masafa marefu na treni za mjini kwa Dar es Salaam kutoka katikati ya jiji hadi Pugu na Ubungo. Bi. Amina amesema kuwa kuna safari tatu asubuhi na tatu jioni kwa treni ya Pugu lakini kutokana na changamoto iliyojitokeza Shirika limeongeza safari kutoka tatu hadi nne kwa asubuhi na jioni.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa Shirika linaongeza idadi ya safari ili kuwahudumia wananchi, hivyo amewaomba kuendelea kutumia huduma za usafiri wa treni za mjini. Bi. Amina amewasihi wananchi kufuata taratibu za usalama ikiwemo kuacha kuning’inia kwenye milango ya treni ili kuepuka ajali.