RASILIMALI WATU; BIASHARA INAYOWEZESHA

May
2025
Kurugenzi ya Utawala na Rasilimali watu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), imesema Rasilimali watu ni biashara inayowezesha kwa kuleta mfumo wa kushirikiana na idara nyingine katika kila jambo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa TRC Bi. Irene Ungani Kyara ,wakati
wa mafunzo ya ndani ya watumishi wa idara ya rasilimali watu na utawala yaliyofanyika Mei 06, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano katika jengo la stesheni ya SGR ya John Pombe Magufuli jijini Dar es Salaam.
Akiongelea lengo la mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala TRC Bi. Irene Kyara alisema kuwa somo kuu ni “Rasilimali watu ni biashara inayowezesha” kwa kuleta mfumo wa idara ya rasilimali watu na utawala kushirikiana na idara nyingine katika kila jambo.
“Tumegawana majukumu ya mtu wa rasilimali watu na utawala kusimamia kila idara kuanzia kuhudhuria vikao vya idara husika, kujua kila kinachoendelea pamoja na kutatua changamoto iliyopo kwenye idara ” alisema Bi. Irene Kyara.
Aidha alieleza pia kuwa mafunzo haya yatawapa mwangaza watu wa rasilimali watu na Utawala kujua ni namna gani ya kufikiri na kua na mabadiliko chanya ya utendaji kazi kwa waajiri na waajiriwa katika utendaji kazi.
Katika hatua nyingine Mshauri mwelekezi wa masuala ya rasilimali watu ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo Prof. Solo Kabeho, alifafanua kwamba mafunzo hayo yatawajengea uwezo na namna ya kuboresha huduma za rasilimali watu na utawala kwa wafanyakazi wa TRC ili shirika liweze kuwa na ufanisi zaidi na kuweza kufikia malengo na mikakati iliyowekwa.
“Mtu wa rasilimali watu na utawala unatakiwa ufuate sheria, kanuni na utaratibu na pia kabla ya kufanya maamuzi ya jambo lolote la mfanyakazi lazima uwe mdadisi na kuona hoja za msingi na pia unaposhughulika na watu unatakiwa kutumia utu na ubinadamu” alieleza Prof. Solo.
Mafunzo hayo yaliyotolewa yataleta weledi katika kazi kwa kutoa huduma ya rasilimali watu na utawala kwa ufanisi na ubora kwa kushirikiana na idara nyingine katika shirika.