Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAIS WA GUINEA - BISSAU ATEMBELEA TRC NA KUJIONEA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI WA TRENI ZA SGR


news title here
22
June
2024

Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau Mhe. Umaro Sissoco Embalo atembelea Shirika la Reli Tanzania - TRC na kujionea Ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa - SGR Juni 22, 2024.

Rais Embalo ambae yuko nchini kwa ziara ya kikazi amelitembelea Shirika la Reli Tanzania kujionea maendeleo na mafanikio katika sekta ya Uchukuzi ikiwemo Ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa na shughuli za usafarishaji wa treni za SGR zilizoanza hivi karibuni.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema kuwa ziara ya Rais Embalo nchini Tanzania inadhihirisha ni kwa namna gani ujenzi wa SGR umehamasisha nchi nyingi za Afrika kuwekeza katika sekta ya usafiri wa reli.

"Kuona Rais wa nchi anatoka nchi nyingine anakuja Tanzania kuona watanzania wamewezaje hilo ni jambo la kumshukuru Mungu na pili kumshukuru Rais wetu Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan aliYetufikisha hapa" amesema Mhe. Kihenzile

Aidha, Kihenzile ameongeza kuwa ujio wa Mhe. Rais Umaro inaonesha umahiri na ufanisi wa utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Reli Tanzania.

"Ujio wa Rais wa Guinea Bissau kwetu inamaanisha tunafanya kazi nzuri ambayo inapendwa na kuonekana na wenzetu kwahiyo tulipo ni pazuri " ameomgeza Naibu Waziri.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa ziara ya Rais wa Guinea Bissau itaongeza ushirikiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Guinea Bissau kupitia ujenzi wa SGR.

" Tunashukuru sana ujio wa Rais wa Guinea Bissau, najua ni maamuzi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Tanzania kumleta mgeni wake na sisi kama Taasisi na bodi yetu ni jambo la fahari ukizingatia yako mashirika zaidi ya 300 ya Serikali lakini Rais Embalo amechagua kuitembelea TRC" amesema Kadogosa.

Ikumbukwe kuwa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa utaleta hamasa katika sekta ya Biashara kati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya wa SADC.