Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAIS WA BURUNDI APANDA TRENI YA MAJARIBIO YA SGR KUTOKA PUGU HADI KWALA MKOANI PWANI


news title here
24
October
2021

Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye atembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha Dar Es Salaam – Morogoro kwa kutumia treni ya uhandisi kutoka stesheni ya SGR Pugu hadi Kwala mkoani Pwani hivi karibuni 23 Oktoba, 2021.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye yupo nchini Tanzania katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi ya Tanzania na Burundi.

Rais Ndayishimiye alipata taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa reli ya Kisasa - SGR kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na kushuhudia ujenzi ulivyokamilika kwa asilimia 94 huku akitembea kwa treni ya uhandisi kutoka stesheni ya pugu mpaka Kwala, mkoani Pwani ambapo alitembelea eneo la hekta 10 ambalo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipatia Serikali ya Jamhuri ya Burundi ili kurahisisha shughuli za usafirishaji.

Mara baada ya kufika eneo la bandari kavu Kwala mkoani Pwani, Rais Ndayishimiye alitoa shukurani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Burundi kwa zawadi kubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa - SGR pamoja na Serikali ya Tanzania kutoa eneo la bandari kavu kwa ajili ya nchi ya Burundi, ambapo amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo itasaidia kujenga uhusiano mzuri wa sekta ya biashara, uchumi na viwanda kati ya Burundi na Tanzania.

‘’Warundi wamepata zawadi kubwa mbili kwanza ni hii reli ya kisasa – SGR, Burundi tulikuwa tunasumbuka sana wafanyabiashara wakitaka kusafirisha bidhaa zao kuleta Buurndi kutoka Dar es Salaam wamekuwa wakitumia muda mwingi pamoja hivyo reli hii ni zawadi kubwa sana kwetu na tutaimarisha uhusiano wa biashara kupitia reli hii. Nimeambiwa kuwa reli ya kisasa itafika kwa siku 1, hivyo bei ya malighafi kwa nchi ya Burundi itapungua’’ alisema Mhe. Rais.

Hata hivyo Rais Ndayishimiye aliweka wazi namna reli ya kisasa itakavyochagiza maendeleo kwa kuokoa muda pamoja na umbali, ‘’Reli itatusaidia kusafirisha bidhaa mbalimbali kwa haraka, salama na bei nafuu. Hapo mwanzo tulikuwa tunatumia gharama kubwa za usafirishaji lakini kwa sasa tutalipa gharama kidogo na hizo pesa tutakuwa tumeziokoa na kwenda kuwekeza kwenye miradi mingine’’ aliongeza Mhe. Rais.

Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameeleza namna Serikali ya Tanzania inavyotekeleza diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana kibiashara na nchi jirani za Afrika katika usafirishaji wa mizigo ambao utakuwa ni tija katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania na barani Afrika.

‘’Kwa upande wa reli bandari hii kavu ya Kwala itaunganishwa kwa reli za aina mbili, kwanza ni reli zamani – MGR, pili reli ya kisasa – SGR. Na kwa sasa tumeanza kujenga jumla ya Kilomita 1.3 zimekwisha kujengwa na zimegharimu milioni 434’’ alisema Waziri Mbalawa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa alibainisha kuwa lengo la mradi huu wa SGR ni kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kwa wingi na kwa muda mfupi ili kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuziunganisha bandari na nchi jirani ambazo hazina bahari.

Tanzania Census 2022