Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAIS SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA MIWILI KATIKA SEKTA YA RELI NCHINI


news title here
05
July
2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ambayo ni mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Tabora – Isaka pamoja na mkataba wa mafunzo kwa vitendo kwa watumishishi wa Shirika la Reli Tanzania - TRC, Ikulu jijini Dar es Salaam Julai 4, 2022.

Mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Tabora – Isaka umesainiwa kati ya TRC na kampuni ya Yapi Merkezi kutoka nchini Uturuki ikiwa ni ukamilishaji wa sehemu ya ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye vipande vitano.

Mkataba wa mafunzo kwa vitendo umesainiwa kati ya TRC na kampuni ya Korea Railways kutoka nchini Korea ukiwa na lengo la kuwapa mafunzo watumishi wa Shirika katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji mara baada ya reli ya kisasa kukamilika na kukabidhiwa kwa TRC.

Aidha, kipande cha Tabora hadi Isaka kina jumla ya kilomita 165 ambapo kilomita 130 ni njia kuu na kilomita 35 ni njia za kupishania. Thamani ya mkataba wa ujenzi ni Dola za kimarekani milioni 900.1 sawa na fedha za kitanzania trilioni 2.094, muda wa utekelezaji ni miezi 42 ikijumlisha muda wa majaribio wa miezi 6

Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi, viongozi wa dini, wakuu wa majeshi, mawaziri na naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wamikoa, wakuu wa wilaya, uongozi wa wizara pamoja na uongozi na wafanyakazi wa Shirika la Reli.

Rais Samia amesema kuwa mikataba iliyosainiwa ni muhimu katika kuendelea mradi wa SGR ambao kwa kiasi kikubwa unakwenda kuleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na kupunguza utegemezi wa wataalamu wa sekta ya reli kutoka nje.

“Mikataba hii ina umuhimu wa kipekee kwakuwa inakamilisha awamu ya kwanza ya reli yetu ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kuanza matayarisho ya kuwajengea uwezo watanzania wa kuendesha na kuisimamia reli yetu badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje” alisema Rais Samia

Mhe. Samia amesisitiza kuwa reli ya kisasa itaunganisha mikoa 9 ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Simiyu na Mwanza lakini pia itaziunganisha nchi za jirani za Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Sudani ya Kusini na nchi nyingine za Afrika. Rais Samia ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Shirika la Reli, Wakandarasi na washauri kwa usimamizi mzuri wa mradi wa SGR.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa thamani ya uwekezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa umefikia trilioni 16 kwa awamu ya kwanza ya Dar es salaam hadi Mwanza na serikali hadi sasa imelipa malipo yote yenye jumla ya shilingi trilioni 6.4 ya malipo ya kazi yote iliyotekelezwa na hukakikiwa ubora wake.

Kadogosa amemshukuru Rais Samia kwa ujasiri wa kuendeleza mradi wa SGR kwasababu unatumia fedha nyingi na kuongeza kuwa mradi wa SGR utaleta manufaa kwa vizazi vijavyo na vitatambua mchango mkubwa uliofanywa na Mhe. Samia akiwa Makamu wa Rais na sasa akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tanzania Census 2022