Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAISI SAMIA AFURAHISHWA KUANZA KWA SAFARI ZA TRENI ZA SGR DAR ES SALAAM - MOROGORO


news title here
14
June
2024

Katika kusheherekea mafanikio ya kuanza safari za treni za SGR ,Daresalaam- Morogoro na Morogoro-Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewalipia nauli wasafiri wote waliosafiri safari ya kwanza Juni 14, 2023.

Akiongea wakati wa safari ya Kwanza ya treni ya SGR kutoka Dar Es Salaam - Morogoro Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe.David Kihenzile amesema kuwa Mhe.Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ujenzi wa miradi ya Kimkakati ikiwemo SGR katika kuleta mageuzi ya kiuchumi haswa kupitia sekta ya Uchukuzi .

"Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipoingia madarakani wengi tunafahamu tulikuwa na ujenzi wa SGR kipande cha kwanza na kipande cha pili pekee, leo tunapozungumza tunaona kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro safari zimeanza hili ni jambo la kihistoria kwa furaha hiyo wakati tunatoka Dar es Salaam Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuelekeza na Mkurugenzi wa TRC ashaanza kutekeleza wale watakaosafiri kwa leo watasafiri buree, kwa mliosafiri leo Rais amelipia" amesema Kihenzile.

Aidha, Mhe. Naibu Waziri amesema kuwa watanzania wanatakiwa kujivunia na kuanza kuona fursa za kiuchumi zilizoko kupitia reli ya SGR na kubuni mbinu za kibiashara kati ya Tanzania na nchi tunazopakana nazo Kama Demokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na Zambia.

"Kwa bara la Afrika reli yetu ya SGR ndio reli ndefu kuliko zote, Duniani tumeshudia mataifa kama China ambao wana takribanI kilomita 40,000 za SGR, wenzetu Hispania wana kilomita takribani 39,000, Japan Wanatakribani 37,000 na Ufaransa wana kama kilomita 27,000 za ujenzi wa SGR, baada ya hapo nchi inayofuata ya tano ni Tanzania yenye takribani kilomita za ujenzi 2102, kwa Afrika ndio nchi pekee inajenga reli ndefu na ya bei nafuu na ya kisasa" alisema Mhe. David Kihenzile.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewataka Watanzania na Wanamorogoro kwa ujumla kutumia usafiri wa Treni ya Kisasa ya SGR ili waweze kuongeza ufanisi katika uzalishaji haswa katika sekta ya Biashara.

"Ushahidi nimeona leo, watu wameondoka Dar es Salaam saa kumi na mbili kamili asubuhi na Saa mbili kasoro dakika kumi (07:50) wako Morogoro, kwa mwendo ukilinganisha na aliyeondoka na basi saa 12 asubuhi Dar es Salaam, sahizi atakua anaitafuta Mlandizi hata Chalinze hajafika, kwamba kwenye muda (time Factor) kuna watu wengi watakua wanaaweza kutoka Dar es Salaam anafika Saa mbili Morogoro na Saa Kumi na mbili jioni anarudi Dar es Salaam anapata masaa kumi ya kufanya Biashara" amesema Mhe. Malima

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameidhinisha kuanza rasmi safari za treni za SGR kutoka Dar es Salaam - Morogoro ikiwa na mabehewa 14 ambapo 11 ni ya daraja la kawaida na matatu (3) ya daraja la Biashara.

"Leo tumeanza rasmi safari za Dar es Salaam - Morogoro, kuna ofa ambayo imetolewa na Mhe. Rais, kama mlivyomsikia Naibu Waziri kwamba wasafiri wetu wamelipiwa na Rais kwa safari hii ya kwanza kwasababu ni jambo kubwa katika Taifa Letu" Amesema Kadogosa.

Safari za awali za treni za SGR zimeanza rasmi kati ya Dar es Salaam na Morogoro Juni 14, 2024 ikiwa ni maandalizi ya kuanza rasmi kwa safari hizo Kati ya Dar es Salaam na Dodoma ifikapo Julai 25, 2024.