Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAIS MUSEVENI ATEMBELEA JENGO LA STESHENI YA SGR LA TANZANITE JIJINI DAR ES SLAAM


news title here
28
November
2021

Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amefanya ziara kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR katika Stesheni ya SGR jijini, Novemba 28, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Uganda yuko nchini Tanzania katika ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Novemba 27 – 28 Novemba 2021. Lengo la ziara hiyo ni kuona maendeleo ya mradi huo wa kimkakati ambapo alipata fursa ya kukagua jengo la Stesheni ya Dar es Salaam ambalo limejengwa kwa mfano ya Madini ya Tanzania, madini ambayo yanapatika Tanzania pekee.

Akihutubia katika ziara hiyo Mhe. Rais Museveni amesema kuwa amefurahishwa na namna nchi ya Tanzania inavyosonga mbele kiuchumi katika kuboresha miundombinu na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, jambo ambalo limechangiwa na mwamko mkubwa ambao watanzania wameupata kwa kufanya kazi na kukuza uchumi wa nchi.

Rais Museveni ameongeza kuwa "Usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni ni bora, rahisi na unaokoa muda zaidi kwa sababu treni ina uwezo wa kusafirisha mzigo mkubwa kwa safari moja na hii itasaidia kukuza uchumi wa nchi zetu za Afrika Mashariki"

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unakwenda kuziunganisha bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania na bandari ya Port Bell nchini Uganda ambazo ni muhimu katika uchumi wa nchi hizo mbili na Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria, kwa kufanya hivyo kutaharakisha zoezi la kupakia na kupakua mizigo na kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari hizo.

Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya reli kwa kujenga reli mpya ya kisasa ili kuliongezea Shirika la Reli ufanisi katika kubeba mizigo.

“Serikali ya Tanzania inawekeza katika uboreshaji miundombinu ya zamani na kujenga miundombinu mipya ya kisasa ili kuendana na uchumi mzuri kwa nchi za Afrika Mashariki" ameongeza Waziri Makame Mbarawa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR ameeleza kuwa kwa sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye urefu wa Kilometa 1219 kwa njia kuu.

Pia Ndugu Kadogosa ameongeza kuwa ujenziwa reli ya kisasa utasaidia kukuza uchumi na utaunganisha kibiashara nchi za Afrika Mashariki kupitia bandari na ziwa Victoria kwa kuokoa muda wa safari na gharama za usafirishaji hadi 40%.

“Usafirishaji wa mizigo kwa njia ya Treni kwa kutumia treni za kisasa utarahisisha zaidi na kuokoa muda, safari moja ya treni itakua na uwezo wa kusafirisha Tani 10,000 kwa safari moja" amesema Ndugu Masanja Kadogosa.

Aidha, Kadogosa amesema kuwa TRC imeweza kurejesha huduma ya usafirishaji wa shehena ya mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Kampala nchini Uganda kupitia reli, pia TRC inaendelea na jitihada za kuboresha huduma za usafiri wa reli kati ya Tanzania na Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Reli Uganda kwa lengo la kuzifaidhisha nchi ya Uganda na Tanzania kupitia Bandari.

“Hivi karibuni miezi miwili iliyopita tumeanza biashara ya mafuta, yanatoka bandari ya Dar es Salaam yanapita ziwa Victoria na kufika Port Bell nchini Uganda, na mpaka sasa tumeshapeleka matenki 72 ambayo ni sawa na Lita Milioni 3,240,000, kwahiyo ni huduma ambayo ilipotea na tumerudisha”

Kadogosa amesema kuwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro umefika zaidi ya 95% , Morogoro – Makutupora ambao umefika 75% pamoja na Isaka Mwanza ambao umefika 3.87%, huku vipande vya Makutupora – Tabora na Tabora – Isaka vikiwa kwenye maandalizi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.

Tanzania Census 2022