Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

RAIS MAGUFULI AZINDUA HUDUMA ZA USAFIRI WA TRENI KATI YA DAR ES SALAAM, TANGA NA ARUSHA


news title here
24
October
2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli azindua rasmi huduma za usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam, Tanga na Arusha, katika Stesheni ya Arusha Oktoba 24, 2020.

Hafla ya uzinduzi imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Majeshi nchini Venance Mabeyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias Kwandikwa, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) Dkt. Leonard Chamuriho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro, wajumbe wa Bodi TRC, Menejimenti, Viongozi wa Dini, Wadau wa TRC, wanahabari na wananchi.

Aidha, katika hotuba yake Mhe. Rais amewapongeza wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kazi kubwa iliyofanywa ya kurejesha huduma za usafiri wa treni za abiria na mizigo uliosimama kwa zaidi ya miaka 30.

Mhe. Rais ameahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Shirika hilo kwa ununuzi wa vichwa vipya vya treni 39 vya njia kuu, Vichwa sogeza 18, Behewa 37 za abiria na Behewa za mizigo 800 na kusema kuwa “Nataka Shirika hili liwe mfano Afrika kwa kuhudumia wananchi wake wakiwemo wanyonge na kufanya biashara, wito wangu kwenu hakikisheni mnafanya kazi na gharama zenu zinakuwa za chini”

“Nawashukuru wafanyakazi wa TRC kwa kazi kubwa mliyoifanya kwa ajili ya Watanzania” alisema Dkt. Magufuli

Naye Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kadogosa alieleza kuwa Mradi wa ufufuaji wa reli ya Kaskazini umetumia zaidi ya Bilioni 14 ambazo ni fedha za serikali, sambamba na hilo kazi ya ufufuaji imefanywa na Wahandisi, Mafundi na Vibarua watanzania ktuoka TRC.

“Thamani ya mradi huu imegharimu zaidi ya Bilioni 10, fedha hii imetolewa na serikali yako lakini pia kazi hii ilifanywa na watanzania wazalendo, wahandisi wetu, mafundi nchundo na vijana wengine zaidi ya 600 ambao ni vibarua” alisema Kadogosa

Kadogosa aliongeza kwa kueleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza huduma za treni katika reli ya Kaskaini kwa kusema kuwa “Hapo zamani reli hii ilitumika sana kusafirisha Kahawa na Sukari kupeleka Dar es Salaam na kuleta Saruji na Mbolea katika mikoa ya Kaskazini, lakini tangu tuanze mpaka sasa tumesafirisha zaidi ya abiria 50,5076 na Tani zaidi ya 26,000 za Mbolea na Saruji”

Ndugu Kadogosa alieleza pia mikakati ya Shirika la Reli kuboresha huduma ya usafiri katika reli ya Kaskazini kwa kununua Behewa za Majokofu ambazo zitawawezesha wakulima wa mbogamboga, maua na wafugaji kusafirisha bidhaa zao kuzipeleka katika maeneo ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi mkuu amemshukuru Mhe. Rais na kueleza baadhi ya jitihada zilizopo kwa kushirikiana na wadau wengine katika huduma za usafiri nchini “Sisi tunakushuru kwa uwekezaji mkubwa unaoufanya, sio kwa kufufua tu bali pia kwa kujenga reli mpya, Mhe. Rais tunashirikiana na Mamlaka ya Bandari, tumewapa sehemu kwa ajili ya kuweka Makontena kwa ajili ya Mizigo, lakini pia kwa kushirikiana na Kampuni ya Huduma za Meli tumepanga kuanza kutumia tiketi moja kwa usafiri wa majini na reli” alisema Kadogosa.