Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​RAIS DKT. SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA UJENZI WA SGR TABORA - KIGOMA


news title here
22
December
2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ashuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR awamu ya pili, kipande cha kwanza Tabora - Kigoma Ikulu jijini Dar es Salaam, Disemba 20, 2022.

Mkataba umesainiwa kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Masanja Kadogosa na Mkurugenzi Mtendaji wa 'China Civil Engineering Construction Corporation' (CCECC) Tanzania Bwana Zhang Junle kwa niaba ya ubia wa kampuni ya CCECC na ‘China Railway Construction Corporation’ (CRCC) za nchini China.

Mkataba unahusisha ujenzi wa kilomita 506 za reli ya kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma ambapo kilomita 411 za njia kuu na kilomita 95 njia za kupishania, Stesheni 10 za abiria na vituo vikubwa viwili (2) vya mizigo Uvinza na Katosho kwa muda wa miezi arobaini na nane (48). Thamani ya mkataba ni dola za Marekani Bilioni 2.21 sawa na Shilingi Tirilioni 5.12 za Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa ujenzi wa reli ya Tabora - Kigoma utaenda kuifungua na kuinganisha Tanzania na nchi jirani ya Congo kupitia usafirishaji wa mizigo na biashara kwa kutumia bandari ya Dar rs Salaam kupitia Uvinza - Msongati mpaka Kindu na kuelekea Congo.

“Reli hii ya Tabora - Kigoma na ile ya Uvinza - Msongati mpaka Kindu ni reli zinazokwenda kuifungua Tanzania na kuiungunisha na DR Congo ambako kuna mizigo mingi inayohitaji kusafirishwa kupitia bandari yetu, Congo kuna machimbo ya madini yenye mizigo zaidi ya tani milioni 150 na mizigo mingine ya kuwezesha migodi hii kufanya kazi, hivyo hii ni fursa” amesema Dkt. Samia

Aidha, Mheshimiwa Rais ameongeza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa nchini umeleta faida nyingi kwa watanzania ikiwemo ajira mbalimbali ambapo mpaka sasa kwa ujenzi unaoendelea wa awamu ya kwanza Dar es Salaam - Mwanza umetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 20,000 na kulipa mishahara takribani bilioni 237.66 za Kitanzania na zabuni zenye thamani ya shilingi Trilioni 1.910 zimelipwa wa makampuni ya wazawa huku kodi ya mapato iliyokusanywa ni shilingi bilioni 949.

“Niendelee kuipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Shirika la Reli Tanzania kwa kusimamia vema ujenzi huu wa SGR, niendelee kuwataka mhakikishe kuwa mnasimamia mradi huu kwa weledi ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, ni matarajio yangu kuwa mtaongeza uzalendo, ubunifu, kujituma na kufanya kazi kwa timu” amesema Mhe. Rais

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini ni muhimu sana kwakuwa sekta hiyo ni chanzo kikubwa cha kuiunganisha nchi ndani na nje na kuleta mapinduzi katika uchumi kwa kuzifungua sekta nyingine katika biashara na uwekezaji.

“Tunatambua azma ya Serikali na msukumo mkubwa uliouweka katika kuhakikisha sekta hii ya usafirishaji inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa, pia tunaitambua azma ya Serikali kuweka miundombinu bora ya usafiri ili kuwezesha ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kama kilimo, madini na utalii vyote vinategemea sekta ya uchukuzi katika shughuli zake” amesema Prof. Mbarawa.

Mtendaji Mkuu wa kampuni ya CCECC Bwana Zhang ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini kampuni ya CCECC kujenga miradi mikubwa hapa nchini, ameahidi kuwa CCEECC itajenga kwa umakini kwa kuunganisha nguvukazi, utaalamu na Teknolojia ya hali ya juu ili kuweza kufikia ubora katika ujenzi wa reli hiyo.

“Sisi CCECC tunaishukuru serikali ya Tanzania kutuamini, Tanzania ni nyumbani kwetu, tunaahidi kujenga SGR ambayo itakua funzo kwa wahandisi wazawa, mradi utakaotengeneza ajira nyingi kwa watanzania, mradi utakaokuwa mfano wa mafunzo kwa wengine na wenye viwango vya hali ya juu” amesema. Bwana Zhang Junlee.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya Tabora - Kigoma unaenda kukamilisha ujenzi wa reli ya kati ya SGR ambapo Tanzania imeweka historia ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kuwa na reli ya SGR ndefu yenye jumla ya kilomita 2,201 pindi itakapokamilika.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania imeendelea kununua vitendea kazi na vifaa mbalimbali ikiwemo mabehewa themanini na tisa (89) ya abiria, vichwa kumi na (19) vitakavyotumia umeme, seti kumi (10) za treni za kisasa (Electric Multiple Unit - EMU) na mabehewa 1,430 ya mizigo na vifaa vya kisasa vya matengenezo ya njia ishirini na nne (24).