Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​PROF. MBARAWA ARIDHISHWA NA UTAYARI KUELEKEA KUANZA KWA HUDUMA ZA SGR DAR ES SALAAM - DODOMA


news title here
03
July
2024

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amefanya ziara kukagua huduma za usafiri katika mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR Dar es Salaam - Morogoro na kuona maandalizi ya kuanza uendeshaji wa huduma za SGR Dar es Salaam - Dodoma, Julai 3, 2024.

Waziri Mbarawa amefanya ziara kwa lengo la kuona utayari na kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuanza uendeshaji wa huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Prof. Mbarawa ameambatana na baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania ambapo alipata fursa ya kusafiri na treni ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, kukagua njia ya reli kuanzia Morogoro hadi Dodoma pamoja na majengo ya Stesheni Kilosa na Dodoma.

"Tumeanza Morogoro sasa hivi tumefika hapa Dodoma, tumekuta kuna mambo mengi kwa asilimia kubwa yamekamilika, lakini kuna mambo machache hayajakamilika ikiwemo ufungaji wa uzio wa Tembo na mkandarasi yupo eneo la kazi na tumejiridhisha baada ya siku nane kazi hiyo itakua imekamilika" alisema Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa ameridhishwa na ukamilishaji wa kazi kwaajili ya kuanza utoaji huduma za SGR Dar es Salaam - Dodoma na kuongeza.kuwa Serikali iko tayari kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

"Kama Waziri mwenye dhamana nimeridhishwa na kazi bila shaka itakapofika Julai 2024 treni itaanza rasmi kutoa huduma Dar es Salaam hadi Dodoma" alisema Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa amelishukuru Shirika la Reli Tanzania kwa kusimamia mradi wa SGR pamoja na Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuhakikisha mradi unakamilika ili wananchi wanufaike na uwekezaji wa kodi zao katika mradi.

Mkurugenzi wa Miundombinu na Ujenzi TRC Mhandisi Machibya Shiwa amesema kuwa Shirika limejipanga kuhakikisha ifikapo Julai 25 huduma zinaanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro

"Sisi kwetu ni faraja kubwa kuona reli inatumika kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro tunaendelea kupata motisha ya kuendelea na ujenzi maeneo mengine" aliongeza Mhandisi Machibya

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dodoma hadi Mwanza na Kigoma ili.kuunganisha mikoa mingine na nchi za jirani kwa lengo la kukuza uchumi. Kuanza kwa huduma za SGR Dar es Salaam hadi Morogoro kunaleta matumaini makubwa kwa watanzania katika kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.